Mwanza. Siku nne tangu Jeshi la Polisi litoe taarifa kuwa kifo cha kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Remigius (52), mkazi wa kijiji cha Karagara wilayani Misenyi Mkoa wa Kagera, kimesababishwa na ajali ya pikipiki, chama hicho kimeibua mapya.
Novemba mosi, 2024, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime kupitia taarifa yake kwa umma, alisema kabla ya Remigius kufariki dunia akitoka kunywa pombe baa, Oktoba 31, 2024, saa 3:00 usiku, alibebwa kwenye bodaboda ndipo akapata ajali na kufikishwa kituo cha afya Minziro, kisha kupatiwa matibabu na baadaye akaruhusiwa.
Kwa mujibu wa Misime, Novemba mosi, 2024, saa 10:20 jioni kulipokelewa taarifa katika kituo kidogo cha Polisi Minziro wilayani humo kuwa Remigius, amefariki dunia akiwa nyumbani kwake, huku akisisitiza kifo chake kimesababishwa na ajali.
Kutokana na taarifa hiyo ya polisi, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Jumatatu Novemba 4, 2024, amesema taarifa ya Jeshi la Polisi kuhusiana na kifo cha kada huyo inaibua maswali.
Miongoni mwa maswali yaliyoibuliwa na Wenje kuhusiana na taarifa hiyo ni pamoja na kutaka kujua hali ya kiafya ya dereva bodaboda aliyekuwa amembeba kada huyo, eneo ilipotokea ajali na namba ya usajili wa pikipiki iliyohusika katika ajali hiyo.
“Jeshi la Polisi lituambie dereva huyo ni nani, yupo wapi na ana hali gani? Taarifa yao haijataja namba ya usajili wa pikipiki iliyopata ajali, watuambie jina la aliyewapa msaada baada ya ajali, halijasema eneo gani ajali hiyo ilitokea, hawajasema jina la baa ambayo marehemu alikuwa anakunywa pombe.
“Wito wetu (Chadema) Jeshi la Polisi liendelee kuchunguza, ili waliohusika na mauaji ya Joseph Remigius watiwe mikononi mwa sheria,” amesema mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa mbunge wa Nyamagana.
Hata hivyo, alipopigiwa simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda kuhusiana na ulipofikia uchunguzi wa suala hilo, alisema tukio limeshatolewa ufafanuzi na msemaji wa jeshi hilo, huku akidokeza kuwa itifaki ya jeshi haimruhusu kuzungumzia suala lililozungumza na kiongozi wake.
“Ni taratibu za kiutendaji jambo ambalo limezungumza na kiongozi wako huwezi kulitolea ufafanuzi, kama kuna mahali panatakiwa kujaziwa nyama ama pataonekana pamepwaya yeye atahitaji ufafanuzi kwangu nitampatia ili alitolee ufafanuzi,” amesema Kamanda Chatanda.
Jitihada za kumpata Misime kuzungumzia sakata hilo pia zimegonga mwamba baada ya simu yake kuita bila kupokelewa. Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kwa njia ya WhatsApp ulionekana kusomwa, ingawa haukujibiwa.