Chanika moto mkali Ligi ya Kriketi U19 

MICHUANO ya Kombe la TCA kwa vijana wa umri wa chini ya miaka 19 iliwasha moto kwenye viwanja viwili jijini Dar es Salaam ambako timu za Chanika Boys na Indian School zilitoka na ushindi mnono.

Timu ya Chanika Boys ilionyesha ujasiri mkubwa baada ya kuifunga KSIJ Red kwa mikimbio 59 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Annadil Burhan mwishoni mwa juma.

Vijana wa Chanika ndiyo walioanza kubeti na kufanikiwa kupiga mikimbio 121 huku wakipoteza wiketi 7 baada ya kumaliza mizunguko yote 20.

Ilikuwa ni mlima mkubwa kwa vijana wa KSIJ kufikia mikimbio 127 baada ya juhudi zao kugota kwenye mikimbio 62 baada ya wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 18 kati ya 20 iliyowekwa na hivyo kuwafanya vijana wa Chanika kushinda kwa mikimbio 59.

Nyota wa mikimbio kwa upande wa Chanika alikuwa ni Athuman Yusuph Nzovu aliyetengeneza mikimbio 26 bila kutoka na Givin Abdallah aliyeongezea mikimbio 14.

Katika mechi nyingine, timu ya Indian School iliwafunga Elite Caravans kwa ushindi mnono wa wiketi 9 katika mchezo uliochezwa pia mwishoni mwa juma.

Elite Caravans ndiyo walioanza kubeti na kufanikiwa kutengeneza mikimbio 60 baada ya wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 16 kati ya 20 iliyowekwa.

Kirahisi kabisa, Indian School waliweza kuvuka alama hizo kwa kutengeneza mikimbio 61 huku wakipoteza wiketi moja na hivyo kushinda kwa wiketi tisa.

Vasu Goyal na Jenil Shah ndiyo walikuwa nyota wa wiketi kwa Indian School baada kila mmoja kupata wiketi 2.

Harsh Khidkikar pia alifanya vizuri kwa upande wa mikimbio baada ya kuitengenezea Indian School mikimbio 16.

Related Posts