EXCLUSIVE: Kinachomtesa zaidi Alphonce Modest hiki hapa, amtaja Mkude, Zimbwe

KATIKA mfululizo wa makala iliyotokana na mahojiano maalumu kati ya Mwanaspoti na nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kuwika na klabu za Pamba, Simba, Yanga, Mlandege, Mtibwa Sugar na timu ya taifa, Taifa Stars, Alphonce Modest, jana tuliona alivyoeleza kiu aliyonayo ya kutaka kuonana na Bilionea wa klabu ya Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji kabla hajaondoka hapa duniani.

Modest aliyekuwa akicheza kwa umahiri beki ya kushoto, amesisitiza anachotaka katika maisha yake kwa sasa ni kukutana na Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi na Rais wa Heshima huyo wa Simba, ili azungumze naye akiwa yupo kitandani akiendelea kujiuguza.

Leo katika mwendeleo wa makala haya, Modest anaweka bayana kitu kingine kinachomtesa kwa sasa ikiwamo kadhia za mitandao ya kijamii, kiasi amekuwa kimya huko kwa lengo la kuepuka maudhi. Kivipi? Endelea naye…!

Modest anasema mashabiki waliokuwa wanapenda kazi yake hawajui kilichojificha nyuma ya mapito yake, hivyo kaamua kukaa kimya ili kulinda heshima yake kuliko kukejeliwa mitandaoni.

“Mfano mazingira haya uliyonikuta nayo, lazima nitaonekana nilikuwa mpenda starehe, ndio maana naishi maisha duni. Kuna wakati nawasikiaga watu wakiongea, jamaa alikuwa na jina kubwa, ila anaishi kimaskini sana najisikia vibaya kwani naona naitukanisha familia na wanaonisema hawafahamu mapito yangu,” anasema mchezaji huyo.

Anasema alinunua kiwanja nyumbani kwao Kigoma ambacho kilikuwa karibu na barabara, lakini baada ya kuanza kupata changamoto, akatokea mtu mwingine aliyesema alitangulia kukilipia.

“Nilikuwa na lengo la kuwajengea wazazi wangu baada ya kuona eneo hili tulilopo ni dogo ambalo pia nililinua. Sasa mwisho wa siku kila kitu nimekosa, kwani sikuwa na nguvu ya kufuatilia tena,” anasema.

Katika chumba chake kuna tv ndogo, ambapo akilipia king’amuzi anakuwa anaangalia soka la ndani na nje, wakati mwingine muvi za Kinaijeria, jambo linalompa faraja na kujiona kuwa na rafiki ama mke.

“Tv ndio mke wangu, ndio rafiki yangu. Kikiisha king’amuzi, basi nabakia mpweke sana. Kulala chini zaidi ya miaka mitano mchana na usiku siyo mchezo ndio maana najiona ifike siku niondoke duniani,” anasema.

Kati ya watu ambao walimsaidia Modest ni pamoja na kiungo wa Yanga, Jonas Mkude, jambo lililomfanya mwandishi wa makala haya kumtumia ujumbe staa huyo wa wana Jangwani ambaye anaamua kupiga simu.

Mkude bila kusita, akapiga ‘video call’ akapewa Modest ili kuzungumza naye jambo lililoibua tabasamu kwenye uso wa mkongwe huyo kuamini kwamba bado anakumbukwa na mdogo wake.

Maneno ya Modest kwa Mkude yalikuwa hivi: “Nashukuru sana bwana mdogo kwa upendo wako. Huwa nafarijika nikikuona katika tv unacheza, nakuombea kwa Mungu azidi kukubariki. Una moyo wa kipekee sana, tofauti na baadhi ya watu katika jamii wanavyokuchukulia.”

Kisha, Mkude alijibu: “Nimefurahi kukuona, nakuombea kwa Mungu akupe afya njema, azidi kukubariki kaka yangu. Hiyo ni mitihani, itapita na utaendelea na maisha mengine ya furaha.”

Baada ya hapo Mkude alituma ujumbe wa maandishi kwa mwandishi aliouandikwa: “Dada Mungu akubariki, kwa kumkumbuka mtu aliyelala kitandani. Ana uhitaji, naamini kupitia mwandiko wako atasaidika na wengi.”

Mazungumzo ya mwandishi na Modest yakaendelea na alipoulizwa kwanini anamshukuru sana Mkude, mchezaji huyo alikuwa mwepesi kujibu,”kuna kipindi Mkude alinitumia Sh500,000 wakati nikijiuguza Dar es Salaam. Alikuwa ananijulia hali na kunipa moyo kwamba yatapita.”

Huku na kule, staa wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella akampigia simu mwandishi baada ya kujua kwamba yupo Kigoma, kisha akaomba kuzungumza na Modest, na mazungumzo yao yakaanza.

Modest: “Kaka nimepokea simu yako kwa heshima kubwa kulingana na kazi ya soka uliyoifanya katika nchi hii. Binafsi kwa uwezo wako sikuwahi kuufikia, nimefurahia sana kukusikia, vipi habari za Morogoro?”

Majibu ya Mogella, “Morogoro naendelea na mapambano ya maisha. Pole kwa changamoto usikate tamaa utapona. Pia mpe ushirikiano huyo binti ili Watanzania waweze kukusaidia hasa kwa wale watakaoguswa na tatizo lako. Wewe ulikuwa mchezaji mkubwa na uliichezea Stars, acha kukata tamaa na maamuzi yako ya kufikiria kifo yasitishe, kwani Mungu anamchukua amtakaye.”

Kisha wakaanza kutaniana hapa na pale kuhusu mambo ya uwanjani. Iliwachukua kama dakika tatu wakongwe hao katika mazungumzo yao.

Nje na Mkude na Mogella, Modest anamtaja katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kidao Wilfred kwamba kila akienda kutembelea Kigoma mara nyingi huenda kumtembelea.

“Alikuja miezi ya hivi karibuni alinipa Sh100,000, hivyo namshukuru. Kuna wakati anapiga simu kunijulia hali. Ukiacha hao wapo baadhi ya wachezaji wa zamani nawasiliana nao,” anasema.

Baadaye mahojiano yakaendelea kuhusiana na maisha yake ya kawaida na soka alivyocheza.

Modest ni miongoni mwa wachezaji waliocheza mechi za watani wa jadi, Simba na Yanga na hapa anasema dabi ya mwaka 1995 ilikuwa ngumu Simba ikishinda mabao 2-1 dhidi ya Yanga.

Mkongwe huyo anasimulia jinsi ambavyo dakika 90 zilivyokuwa za nguvu.

“Umeona kikosi cha Simba kilivyo na damu changa na Yanga ilivyo na wachezaji wakongwe, sasa kipindi hicho Simba tulikuwa watu wazima na Yanga ilikuwa na damu changa, hivyo ilikuwa ni mechi ya kasi na kutumia mbinu na akili,” anasema.

“Unajua unapocheza na damu changa wanakuwa wanapambana kuonyesha uwezo ili waanze kukubalika na mashabiki, hivyo tulichokifanya sisi ilikuwa ni kutumia akili zaidi na mbinu tukapata matokeo, ndio maana nasema sitaisahau katika maisha yangu.

“Ninaowakumbuka katika kikosi cha Yanga walikuwa kina Edbily Lunyamila, Sekilojo Chambua na Akida Mapunda angalau hao walikuwa wakubwa, ila wengi wao walikuwa wadogo zaidi.”

Kipindi wakati anacheza, Modest anasema alikuwa anaamka saa 12:00 asubuhi, anafanya mazoezi ya kupandisha mlima kisha anaanza kukimbia raundi 12 uwanjani akimaliza anapumzika saa moja, kisha anaunga na mazoezi ya timu yaliyokuwa yanafanywa kuanzia saa 2:00 hadi 4:00 asubuhi.

“Tukimaliza mazoezi ya timu nilikuwa nakunywa kikombe kimoja cha uji wa ulezi, kisha nusu chupa ya chai ya maziwa kisha napumzika. Ikifika saa tisa nilikuwa nafanya mazoezi yangu binafsi saa 10:00 hadi 12 jioni nafanya ya timu, nakwenda kupumzika. Ikifika saa 2:00 usiku nilikuwa nakwenda kufanya mazoezi kama masaa mawili, narudi kambini, naoga, nakula kisha nalala.”

Modest anasema, “ndio maana nilikuwa na pumzi, kasi na nguvu. Niliocheza nao unaweza ukawauliza wakakuambia nilikuwa mtu wa aina gani. Binafsi siwezi kujieleza sana, uwanjani inabidi akuelezea mtu mwingine.”

Mkongwe huyo anamtaja nahodha wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kwa aina ya uchezaji wake akiona unataka kukaribiana na wake, ingawa wanatofautiana miili.

“Ingawa mifumo yao ya sasa ya 4-3-1 ni tofauti na zamani, Tshabalala anachotakiwa kufanyia mazoezi zaidi anapopanda kushambulia asisahau jukumu lake la kukaba. Tofauti yangu na yeye mimi nilikuwa kipande cha mtu,” anasema.

Mbali na hilo anazungumzia uwepo wa wachezaji wa kigeni katika Ligi Kuu ulivyo msaada kwa wazawa, ambao wakicheza timu ya taifa wanapokutana na wapinzani wao hakuna kinachowastajabisha.

“Inawasaidia sana wanapocheza michuano ya kimataifa. Wanakuwa wamepata uzoefu kupitia wageni wanaocheza nao katika ligi,” anasema Modest.

“Nakumbuka zamani tulikwenda kucheza Libya tukakutana na mchezaji aliyetoka kuchukua uchezaji bora wa dunia, George Weah alikuwa kipande cha mtu, yaani wachezaji tunamshangaa. Unaingia uwanjani unawaza mara mbilimbili jinsi ya kukabiliana naye.”

Anaongeza kuwa, “ilikuwa mwaka 1995 kama sikosei ndio maana nasema kitendo cha uwepo wa wachezaji wa kigeni kinasaidia sana wazawa kuzoea.”

Ukiachana na hilo, Modest anawapa ushauri wazawa kuwa waangalifu na umarufu unaoweza kuwajenga au kuwabomoa katika maisha yao.

“Umarufu ni mzigo mzito lazima mchezaji ajifunze kuwa mtulivu, angalau wenzao (yaani wao) hakukuwepo na mitandao ya kijamii kama ilivyo sasa ambapo kila kitu chao kwa sasa kinakuwa wazi. Wasipokuwa makini mwisho wa siku umarufu unaweza ukawaumiza.”

Related Posts