Hakuna ongezeko la maambukizi ya Mpox – DW – 04.11.2024

Katika wiki za hivi karibuni, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeripoti maambukizi kati ya 200 hadi 300 yaliyothibitishwa na maabara kila wiki, kulingana na shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO.

Kiwango hicho kimepungua kutoka karibu visa 400 vilivyokuwa vikiripotiwa kila wiki mnamno mwezi Julai. Kushuka huko kwa maambukizi kunashuhudiwa pia katika eneo la Kamitunga, mji maarufu kwa machimbo ya madini mashariki mwa Kongo kulipoibuka kisa cha kwanza cha maambukizi hayo.

Soma zaidi: Chanjo ya mpox kuchukuwa muda mrefu zaidi Kongo

Shirika la Afya duniani liliweka wazi mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa, ni asilimia 40% hadi 50 pekee ya wanaohisiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya mpox ndiyo wanaopimwa, na kuwa bado virusi hivyo vinaendelea kusambaa katika baadhi ya maeneo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na mahali pengine ikiwemo Uganda.

Wakati madaktari wakionekana wenye matumaini kutokana na kushuka kwa maambukizi katika baadhi ya maeneo ya Kongo, bado haijawa wazi ni aina gani ya mgusano kati ya mtu na mtu unaochochea kusambaa kwa mpox.

Idadi ndogo ya chanjo ni changamoto kwa mapambano dhidi ya mpox

Pamoja na hilo wataalamu wa afya  wamekuwa wakisikitishwa na idadi ndogo ya chanjo zilizopokelewa katika taifa hilo la Afrika ya Kati.

Homa ya mpox
Mmoja wa waathiriwa wa mpox akipatiwa matibabu huko Goma, DRCPicha: Xinhua/IMAGO

Siku kadhaa zilizopita, WHO lilitangaza kuwa zaidi ya watu 50,000 wamepatiwa chanjo dhidi ya mpox, katika mataifa ya Rwanda, na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, hatua iliyopongezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Tedros Ghebreyesus.

Mkuu huyo wa WHO alisema kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuidhibiti homa ya mpox, na ni sehemu ya mpango mkakati wa pamoja wa WHO na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Afrika (CDC).

Aliongeza kuwa ni muhimu kusisitiza kuwa chanjo ni sehemu moja tu ya mpango huo pamoja na kutafuta walioambukizwa, kufuatilia mawasiliano, kuzuia na kudhibiti, huduma za hospitali, na kuripoti pale panapohisiwa kuwa nahatari ya maambukizi pamoja na vipimo.

Pamoja na matumaini yanayotokana na kutokuongezeka kwa maambukizi ya homa ya mpox, wanasayansi wanasema juhudi za haraka za kutoa chanjo katika bara zima la Afrika  zinahitajika ili kuzuia kuibuka kwa aina mpya ya virusi hivyo kama ile iliyogunduliwa mapema mwaka huu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya miezi mingi ya maambukizi ya ngazi ya chini.

 

Related Posts