Wakati huo huo jeshi la Israel limedai kuwa limemuuwa kamanda mmoja mkuu wa kundi la Hezbollah anayedaiwa kuhusika na mashambulizi ya makombora kusini mwa Lebanon.
Katika taarifa, wizara ya mambo ya kigeni ya Israel imesema kuwa imeufahamisha Umoja wa Mataifa kuhusiana na kusitishwa kwa mahusiano yake na UNRWA katika mkataba uliotiwa saini mwaka 1967.
Hatua hiyo ya Israel inaonekana ni mwendelezo wa sheria iliyopitishwa mwezi uliopita iliyotaka kuzuia shirika hilo kutofanya kazi nchini Israel.
Kusambaratika kwa misaada ya kiutu Gaza
Israel inasema shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeingiliwa na wanamgambo wa Hamas, madai ambayo UNRWA yenyewe inayakanusha na kudai kuwa inachukua hatua kuhakikisha kwamba haiegemei upande wowote katika utekelezaji wa majukumu yake.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa kwa upande wake limesemahatua hiyo ya Israel itasababisha kusambaratika kwa kazi ya misaada ya kiutu katika Ukanda wa Gaza unaokabiliwa na vita.
UNRWA hutoa huduma za elimu, afya na huduma zengine za kimsingi kwa wakimbizi wa Palestina.
Huku hayo yakiarifiwa jeshi la Israel limesema leo kuwa limemuua kamanda mmoja mkuu wa Hezbollah ambaye linamtuhumu kwa kusimamia mashambulizi ya maroketi na makombora dhidi ya vikosi vya jeshi la Israel kusini mwa Lebanon.
Jeshi hilo limesema kuwa Abu Ali Rida ndiye kamanda aliyeuwawa bila kutoa taarifa kamili ya ya lini alipouwawa.
Katika wiki za hivi karibuni Israel imewauwa makamanda kadhaa wa kundi hilo la Hezbollah akiwemo mkuu wa zamani Hassan Nasrallah.
Israel kuingia ardhi ya Syria mara ya kwanza
Kwengineko Jumapili, jeshi hilo la Israel limesema lilifanya uvamizi wa ardhini nchini Syria na kumkamata raia wa Syria waliyemtambulisha kama Ali Soleiman Al-Assi ambaye wanadai anahusika na mitandao ya Iran.
Hii ndiyo mara ya kwanza katika vita hivi, Israel kutangaza kwamba vikosi vyake vimefanya operesheni katika ardhi ya Syria.
Israel imefanya mashambulizi ya makombora mara kadhaa nchini Syria katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ikiwalenga wanamgambo wa Hezbollah na maafisa kutoka Iran ila haijawahi kuweka wazi kwamba vikosi vyake vimeingia katika ardhi ya Syria.
Serikali ya Syria haikuthibitisha mara moja tangazo hilo la Israel ila kituo kimoja cha redio nchini humo ambacho kinaiunga mkono serikali, kiliripoti kwamba vikosi vya Israel vilifanya “operesheni ya utekaji nyara” kikimlenga mtu mmoja kusini mwa nchi hiyo.
Wakati huo huo maafisa wa Palestina wamesema kwamba Waisraeli waliokalia ardhi yao wameyateketeza magari huko Ramallah katika Ukingo wa Magharibi usiku wa kuamkia leo.
Tukio hilo linadaiwa kutokea kilomita chache tu kutoka makao makuu ya Mamlaka ya Palestina.
Vyanzo: AFPE/APE/DPAE