Kiboko mharibifu mazao ya wakulima Magu auawa, wananchi wagawiwa nyama

 

KIBOKO aliyehatarisha maisha ya watu katika Kijiji cha Ilungu Kata ya Nyigogo wilayani Magu mkoani Mwanza, ameuawa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) baada ya kuvamia mashamba ya wakulima wanaofanya shughuli za kilimo cha mpunga na mahindi katika kitongoji cha Moa wilayani humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Magu, Mwanza … (endelea).

Tukio hilo limetokea jana tarehe 3 Novemba baada ya wananchi hao wanaolima kando ya Ziwa Victoria kushindwa kumdhibiti kiboko huyo na hivyo kuomba msaada TAWA ambao walifanikiwa kumuua kwa kumpiga risasi.

Wakizungumza na waandishi wa Habari baada ya Afisa Mifugo wa kata hiyo ya Nyigogo, Hamis Gido kudhibitisha kuwa nyama hiyo ni salama kwa matumizi ya binadamu, baadhi ya wananchi wameishukuru Serikali kwa kuwatatulia changamoto hiyo.

Wamesema eneo hilo pamekuwapo na usumbufu wa kiboko mara kwa mara lakini sasa kutokana na kiboko huyo mmoja kuuawa wanaamini hata wengine waliokuwa karibu watakimbia.

Mmoja wa wananchi hao, Pungwe Wilson ambaye pia ni mkulima amesema kwa muda mrefu pamekuwa na kilio cha wananchi kuhusu wanyama waharibifu wanaotokea kwenye ziwa Victoria.

“Lakini sasa tunaishukuru Serikali kwa kumuua mnyama huyu ambaye pia amekuwa hatari hata kwa Maisha yetu sisi wakuliam,” amesema Wilson na kuungwa mkano na wananchi wengine wakiwamo Magina Mbute na Ngubi Mega.

Awali Askari wa Uhifadhi Mwandamizi kutoka TAWA, Loiruck Moses alisema wamefanikiwa kukabiliana na mnyama huyo ikiwa ni zoezi endelevu la kuwadhibiti Wanyama waharibifu.

Aidha alitoa wito kwa wananchi pindi wanapokabiliana na wanyama pori wanapoonekana mahali popote watoe taarifa ili askari wafike kukabiliana na Wanyama hao.

Naye Afisa Mifugo wa kata ya Nyigogo, Hamisa Gido alisema ni suala lililozoeleka katika maeneo mengi pindi mnyama kiboko anapouawa na nyama yake kupimwa na kuonekana haina dosari yoyote, hugawiwa kwa wananchi ili wapate kitoweo.

Mhifadhi Wanyama pori wilaya ya Magu, Christopher Christian alisema Wanyamapori hao wamekuwa wasumbufu kwa wananchi wa Kijiji hiyo lakini wanaishukuru TAWA kwa kushirikiana Pamoja kudhibiti mnyama huyo.

About The Author

Related Posts