Kuku hai wanavyotumika kusafirisha dawa za kulevya

Dar es Salaam. Kila siku mbinu mpya zinabuniwa ili kukwepa vyombo vya dola; hivyo ndivyo unavyoweza kuelezea taarifa za wauzaji wa dawa za kulevya wanaotumia kuku wa kienyeji kusafirisha dawa za kulevya aina ya kokeni.

Taarifa kutoka vijiji vilivyopo mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ya Kenya, zinadai kuwa dawa hizo hufungwa katika vipakiti vidogo (kete) huku ikielezwa kuwa kuku mmoja huweza kusafirisha kati ya gramu 250 na 300. Na kuku huingizwa kete hizo kupitia njia ya haja.

“Hiyo ndio deal (mpango) kwa sasa. Shaba zinapita ila sio sana. Sasa hivi ni biashara ya kokeni, inaingia nchini kwa wingi kupitia njia za panya na wanaziweka kwenye kuku wa kienyeji ndio wanapita nao,” kilidokeza chanzo chetu.

Mwananchi lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Saimon Maigwa azungumzie taarifa hizo naye alisema wanaendelea kuzichunguza ili kubaini ukweli wake na watashirikiana na kitengo cha dawa za kulevya.

“Ninashirikiana na vyombo vya usalama, ikiwemo Ofisi ya Kamishna wa Dawa za Kulevya Tanzania, ili kuchunguza taarifa hizi na kuweka mitego kwa lengo la kuwakamata wanaotumia njia hizo za panya,” amesema Kamanda huyo.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, kuku hao huingia nchini kupitia maeneo ya Kitobo na Madarasani katika Wilaya ya Moshi na Mnoa wilayani Mwanga kisha kusafirishwa kwa pikipiki kupitia njia za panya hadi njiapanda ya Himo.

Baadaye kuku hao kwa sehemu kubwa husafirishwa kwenda Jiji la Dar es Salaam na husafirishwa kama kuku wengine wa kienyeji wanavyosafirishwa kutoka maeneo mengine ya Mkoa wa Kilimanjaro kama Kwasadala na vijiji vya Wilaya ya Hai ambako kuna ufugaji mkubwa wa kuku hao.

“Wale kuku waliobebeshwa dawa wanawaweka alama maalum na wanalishwa uji mlaini wa unga wa ugali ambao huchanganywa na drip water (maji ya wagonjwa hospitalini) ili kuwapa nguvu ya kuhimili muda mrefu,” kimeeleza chanzo hicho.

Kulingana na vyanzo mbalimbali katika maeneo ambayo kuku hao huingilia, wanadai baada ya kufika jijini Dar es Slaam, Moshi na Arusha na miji maarufu, huchinjwa na dawa kutolewa kisha kuku huuzwa kama kitoweo.

“Tenga la kubebea huwa linatengenezwa kuruhusu tu mtu kuona ni kuku, lakini huwezi kuingiza mkono kuwashika. Wanachofanya wanaweka mapumba ya randa ili ikitokea amekunya, zile kete zinaishia kwenye mapumba,” imedokezwa.

Taarifa zinadai baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji na mgambo ambao kuku hao hupitia kabla ya kufika njiapanda ya Himo, wapo katika mfumo wa malipo ya wasafirishaji na hulipwa ili kusaidia kusafisha hali ya hewa njia nzima.

“Kama kuna tenga linakuwa na kuku walioshindiliwa hizo dawa, utajua tu maana utaona pilika pilika fulani hivi kuanzia hapo mpakani zinapovushwa tu. Baada ya hapo usalama ni mzuri kwa sababu sio rahisi kushtukiwa,”ameeleza mwananchi mmoja.

Chanzo kingine kimedokeza katika tenga moja, wanaweza kuwepo kati ya kuku 10 hadi 50 lakini sio wote wanaokuwa wameshindiliwa dawa hizo, bali ni wachache na huweza kusafirisha  jumla ya gramu 3,000 hadi 4,000.

Tume yajipanga kukabili uhalifu

Hata hivyo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo naye alipotafutwa na Mwananchi azungumzie hilo, amesema wameanzisha divisheni ya sayansi jinai katika kukabiliana na mbinu za kisasa za usafirishaji wa dawa za kulevya.

“Itakuwa inahusika na dawa zote na kemikali na kubaini mbinu zote zinazotumiwa na wasafirishaji kwenye viwanja vya ndege, mipaka na maeneo yote na sasa hivi tupo kwenye mchakato wa kupata wataalamu,” amesema.

Katika maelezo yake, Jenerali Lyimo amesema wataalamu hao ni waliobobea katika eneo hilo la haki jinai watapelekwa kwenye mipaka na maeneo mengine wanayohisi kuna uvushwaji wa dawa za kulevya.

“Tumeshaanzisha kanda tano,tayari tumeshapeleka wataalamu na katika kila kanda inakuwa na mikoa mitano na kunakuwa na mtu anayeshughulika na maeneo hayo na tunapeleka mipaka yote,”amesema.

Amesema katika kuwezesha ufanisi wa utendaji kazi,watanunua mashine za kisasa ambazo hazihitaji kuchukua dawa na kupima kama dawa imewekwa kwenye meno inawekwa kamkono kake na inasoma kama kuna dawa.

“Mashine hiyo ina uwezo hata ukigusisha kwenye chupa inasoma, tayari tumenunua mashine ya majaribio tumeijaribu inafanya kazi vizuri hata ukibeba gunia la mchele au gunia unaishikiza na inasoma,”amesema.

Amesema mashine hiyo moja thamani yake ni Sh250milioni huku akieleza suala la ukaguzi litakuwa linafanyika kwa urahisi zaidi mipakani kutokana na ujio wa teknolojia ya mashine hizo.

“Tunataka kukabiliana na mbinu mpya ya uingizwaji wa dawa za kulevya kwakuwa wanakuja na mifumo mipya kila siku kuna wanaotumia mbao na laptop.

“Kuna wanaosafirisha kwa kutumia soda kwa kuweka chini ya chupa ya soda, kuna wanaotumia wanyama kuna wakati wanavusha ng’ombe wakiwa wamemuwekea na kwenda kutoa mbele ya safari,” amesema Lyimo.

Lyimo amesema kwa sasa wamebaini mbinu nyingine mpya ya kutumia meno.

Amesema mtu anang’olewa meno yote na kutengeneza ya bandia yanayokuwa na nafasi kwa ndani na yanajazwa kokeni.

“Kokeni ni dawa inayosafirishwa kwa kiwango kidogo sana, tofauti na heroini ambayo huwezi kutumia mbinu hizo, kwa kuwa inahitajika kwa wingi, Kokeni ni kali sana kiasi kwamba mtu anahitaji kidogo sana kupata kilevi,” amesema.

Amesema mtu hata akisafirisha gramu 100 anawauzia watu wengi, ndiyo sababu ya baadhi ya watu huridhia kung’olewa meno na kuwekewa meno ya bandia hata wakicheka huwezi kubaini.

Licha ya vyombo vya dola likiwamo Jeshi la Polisi Mkoa Kilimanjaro kupata mafanikio katika ukamataji wa mirungi, bado shehena kubwa huingia nchini kupitia maeneo ziliko njia hizo za panya.

Tofauti na Kokeni ambayo kwa sehemu kubwa husafirishwa kwenda kwenye miji yenye viwanja vya kimataifa vya ndege na baadaye kusafirishwa kwa siri kwenda nje ya nchi, mirungi husafirishwa kwenda maeneo mbalimbali ya nchi ikiwamo Mkoa wa Dar es Salaam.

Maeneo mengine ambayo mirungi hiyo husafirishwa ni Moshi, Himo, Mwanga, Same na Bomang’ombe mkoani Kilimanjaro ambapo hutumika kama njia kwenda jijini Dar es Salaam na mikoa ya Manyara na Dodoma kwa ajili ya matumizi.

Tofauti na Kokeni ambayo hufungwa kwenye kete, mirungi hufungwa kwenye mabunda na kuwekwa kwenye mifuko ya sandarusi au magunia na kusafirishwa kwa njia ya barabara kwa kutumia mabasi na magari binafsi ya watu au taasisi.

Usafiri mahsusi unaotumika kubeba mirungi kutoka mpakani hadi njiapanda ya Himo, mji wa Himo na Chekereni kupitia njia za panya ni pikipiki na baadaye kuhamishiwa kwenye magari na mabasi, ambayo baadhi yalishanaswa na polisi.

Kifungu cha 15A(1) cha sheria ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya sura ya 95 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019, kinaeleza kuwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya,  atatumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Lakini kifungu kidogo cha 29 (c) kimefafanua kuwa kwa minajili ya kifungu hicho, mtu atakuwa ametenda kosa hilo kama mtu huyo atakuwa amesafirisha mirungi au bangi yenye uzito usiozidi kilo 50 za dawa hizo.

Sheria inataka kutaifishwa kwa chombo kilichotumika kusafirisha dawa za kulevya, lakini tangu wasafirishaji wa dawa hizo kubadili mbinu na kutumia mabasi, hakuna basi hata moja limewahi kutaifishwa kwa kukutwa likisafirisha dawa hizo.

Wilaya ambayo nayo imekuwa ikitumiwa na wasafirishaji wa mirungi kuingiza dawa hizo kutokea nchi jirani ni wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro ambapo mirungi huingia kupitia Tarakea, Usseri, Holili na vitongoji vya mpakani.

Kata ya Njoro katika Manispaa ya Moshi inahesabika kama makao makuu ya watumiaji wa dawa za kulevya aina ya kokeni na heroni ambapo baadhi ya vijana wake kwa waume, hutumia dawa hizo kwa njia mbalimbali.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiriche, David King’ola amesema wasafirishaji hao wanatumia akili na mbinu tofauti; hawajawahi kubaini mbinu wanayotumia kuvusha dawa hizo.

“Inawezekana ni kweli watu wanavusha dawa hizo kwa mfumo huo kwa sababu hatujawahi kufanya operesheni za aina hiyo ila biashara ya kuku hapa inafanyika kwa wingi na ili tuwabaini tunategemea tupate kwa fununu,” amesema.

David amesema katika mpaka huko kuna kuku wanaotoka Kenya kuja Tanzania wakiwa wamebabwa kwenye makasha (matenga), huku akieleza kitongoji chake ni njia ya kupitishia.

“Kitongoji changu kimepakana na Kitongoji cha Kifula au Masaini cha Kenya; kuna mwingiliano mkubwa na ni vigumu kubaini na mwaka juzi polisi walitoka Dar es Salaam kuja kukamata kokeni hapa,” amesema.

Alisema mfumo waliotumia polisi hao ni mgumu si rahisi kwa mtu wa kawaida kuelewa na ili kuwatia mbaroni,  lazima upate taarifa wanakotoka na wanakokwenda.

“Mpaka wetu ni mkubwa na una vichochoro zaidi ya  800 na unaenda kupakana hadi Wilaya ya Mwanga na si rahisi askari kuimarisha ulinzi maeneo yote,” amesema David.

Wataalamu wa mifugo watoa neno

Akizungumza na Mwananchi, mtaalamu wa mifugo, Edwin Bwambo amesema ikitokea kuku ameingiziwa kitu kwenye mfumo wake wa haja, anaweza kupata madhara kiafya kwa kuwa utumbo wao ni mdogo.

“Iwapo kitu hicho kitaingizwa na kikapasuka itakuwa mbaya zaidi na anaweza kufa,” amesema.

Hivyo, ,amesema kama ataingizwa kitu ambacho hakina ncha na kidogo sana kulingana na utumbo wake na kama ni laini, kinaweza kuingia na baadaye akakitoa kwa haja.

Daktari wa Mifugo, Godfrey Mbasa alisema kama analishwa pumba na ugali anaweza kuchukua hadi saa nane hadi sita,  huku akieleza wakilishwa vyakula laini kama uji anaweza kukaa hadi saa 12.

“Wakiwekewa vitu kwenye mfumo wa haja kama sumu anaweza kufa na madhara mengine huwa inategemeana na ukubwa wa kitu anachoingiziwa na kimefungwa kwa material gani ya kuyeyuka au si yakuyeyuka,” alisema.

Alisema kwenye mfumo wa haja wa kuku,  kuna kuwa na unyevuunyevu, lakini akiingiziwa kitu aina ya chuma ni rahisi kwao kupata vidonda.

Related Posts