Makocha wanavyogeuka wazazi | Mwanaspoti

KATIKA ulimwengu wa soka makocha wamekuwa wakichukua kazi ya kuwafundisha wachezaji, lakini pia ni kama walezi wao.

Hiyo inatokana na namna ambavyo muda mwingi wanakuwa pamoja. Hii inalinganisha na masuala ya shuleni ambapo walimu ni kama wazazi kwa wanafunzi.

Septemba 21, 2021, nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo alifichua namna ambavyo Sir Alex Ferguson alikuwa zaidi ya kocha kwake akimchukulia kama baba yake.

Ronaldo ambaye dunia inamtambua kwa kuwa nyota mwenye mabao mengi zaidi upande wa timu za taifa wanaume akifunga 133, alisajiliwa na Ferguson mwaka 2003 akitokea Sporting Lisbon ya kwao Ureno.

Nyota huyo mwenye Tuzo tano za Ballon d’Or, ameitumikia Manchester United kwa vipindi viwili tofauti.

Alianza mwaka 2003 hadi 2009 akiwa chini ya Ferguson, kabla ya kuhamia Real Madrid (2009–2018), kisha Juventus (2018–2021), akarejea Manchester United (2021–2022) na sasa yupo Al Nassr tangu mwaka 2023.

Wakati anarejea United mwaka 2021, Ronaldo alisema: “Kama kila mtu anavyojua, tangu niliposaini Manchester United nilipokuwa na umri wa miaka 18, Sir Alex Ferguson alikuwa ndiye ufunguo wa mafanikio yangu.

“Kwangu, Sir Alex Ferguson ni kama baba katika soka. Alinisaidia sana, alinifundisha mambo mengi, na kwa maoni yangu, alifanya jukumu kubwa kwa sababu ya uhusiano tulionao, tunaendelea kuwasiliana kila wakati.

“Ninampenda sana kwani amekuwa ufunguo wa mimi leo hii kuwa katika nafasi niliyopo.”

Achana na hayo ya Ronaldo. Makocha wa soka katika ngazi zote wanatumika kama viongozi, nguvu inayosaidia kuleta mafanikio kwa timu. Wako hapo kusimamia wachezaji kama wazazi wao, katika hali hiyo, kocha anaonekana katika macho ya mchezaji kama mshauri au baba kwenye familia.

Kocha Mkuu wa Chuo Kikuu cha Oklahoma State cha nchini Marekani, Mike Gundy anasema anawasimamia wachezaji 135 kama watoto wake.

“Wanahitaji kukuamini, wakupende na wajue kuwa unawapenda na kuwajali, kisha watakusikiliza,” anasema Gundy.

Kama ilivyo kwa baba mzuri, pia kocha mzuri ni yule anayewajua wachezaji wake na anajua wapi watafanikiwa au wanahitaji msaada kiasi gani.

Kocha Gundy anabainisha kwamba: “Mimi kwa sasa vijana wangu wananichukulia kama mshauri zaidi kuliko kuniona kama kocha.”

Kufundisha vijana kuna majukumu mengi na changamoto na kocha wa Shule ya Sekondari ya Pearl-Cohn huko Marekani, Tony Brunetti anasema mbinu za nidhamu zimebadilika katika miaka kumi aliyokuwa akifundisha.

“Nafikiri si mkali kama nilivyokuwa nilipoanza kuwa kocha mkuu,” Brunetti anasema na kuongeza:

“Nilikuwa mkali sana kwa wale vijana na walikuwa na uwezo wa kuvumilia. Siku hizi unahitaji kufanya mambo kwa njia tofauti.”

Hivi karibuni wakati sakata la mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize alipokuwa akihusishwa kutakiwa na Wydad Casablanca ya Morocco, iliibuka ishu ya Kocha Miguel Gamondi kusimama kama baba mbele ya mshambuliaji huyo.

Kocha huyo Muargentina, alibainisha kwamba amekuwa akikaa na kuzungumza na mchezaji huyo ili kumshauri masuala mbalimbali ya kisoka.

“Clement ni kama mwanangu. Nilikuwa mtu wa kwanza kumtetea na kumlinda. Kwa sasa anajisikia vizuri kuwa Yanga. Watu wanampenda ndani ya klabu, pia kama kocha namuelewa vizuri, nafikiri naweza kumsaidia sana kukua,” alisema Gamondi.

Hata pale Simba, Kocha Fadlu Davids katika kuwasimamia wachezaji wake analichukua jukumu hilo kama mzazi.

Miongoni mwa wachezaji waliowahi kuthibitisha hilo ni Edwin Balua, Ladack Chasambi na wengineo ambao wanajiona bado wana safari ndefu katika suala zima la kucheza mpira wa miguu.

Inafahamika kwamba mzazi ni mtu anayeheshimiwa zaidi na mtoto wake, hivyo heshima ikitawala katika timu yoyote bila shaka mafanikio hayajifichi.

Wachezaji wakimchukulia kocha wao kama mzazi inakuwa rahisi kufanya kile wanachofundishwa lakini ikiwa tofauti, lazima kuwe na tatizo.

Makocha wengi waliofanikiwa katika ufundishaji wao walitanguliza ukaribu na wachezaji wao.

Jose Mourinho pale Chelsea aliwafanya wachezaji kama watoto wake na kweli wakampa mafanikio kwa muda mfupi.

Tazama Didier Drogba na hata Frank Lampard walivyokuwa wakipambana ndani ya uwanja, hiyo yote ilikuwa ni kutotaka kumuangusha Mourinho.

Lakini timu hiyohiyo ya Chelsea ilipokuwa chini ya Kocha André Villas-Boas, mengi yaliibuka ikielezwa kwamba wachezaji hawakuwa wakimuheshimu kocha wao. Kutoka Juni 2011 hadi Machi 2012, ilitosha kwake kukaa Stamford Bridge, akatimuliwa.

Related Posts