Mwalwisi akomalia safu ya ulinzi

KATIKA kuhakikisha TMA inafanya vizuri katika Ligi ya Championship msimu huu, kocha mkuu wa kikosi hicho, Maka Mwalwisi amesema mkakati uliopo kwenye benchi lao la ufundi, ni kufanyia kazi udhaifu walionao hasa eneo la kujilinda.

Mwalwisi alisema hadi sasa safu ya ushambuliaji imeonyesha matumaini makubwa kwao lakini eneo la kujilinda limekuwa na changamoto.

“Washambuliaji wanafanya kazi yao vizuri kwa michezo tuliyocheza, ila safu ya ulinzi bado imekosa muunganiko mzuri ndio maana tunafunga lakini tunaruhusu pia, tunapaswa kuonyesha mabadiliko hayo kwa haraka ili kuendana na ushindani uliopo.”

Kocha huyo aliongeza, licha ya washambuliaji wa kikosi hicho kufanya vizuri, wanapaswa kuongeza juhudi zaidi, kwani viungo wa timu hiyo wanatengeneza nafasi nyingi za kufunga hivyo ni jukumu lao kuzitumia ili kutengeneza motisha kwao.

Kabla ya mchezo wa jana wa kikosi hicho dhidi ya watani zao wa jadi Mbuni zote za jijini Arusha, TMA na Geita Gold ndio timu pekee hadi sasa katika Ligi ya Championship kati ya 16 zinazoshiriki ambazo zilikuwa hazijapoteza mchezo wowote wa ligi msimu huu.

Related Posts