PINDA ASHIRIKI MAADHIMISHO YA MIAKA 30 YA UMOJA WA WATANZANIA BOTSWANA

Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda ameshiriki Maadhimisho ya miaka Thelathini ya kuanzishwa kwa Umoja wa Watanzania wanaoishi nchini Botswana (ATB) yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Botswana na Jumuiya hiyo yaliyofanyika jijini Gaborone tarehe 2 Novemba, 2024.

Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Pinda amesema Serikali ya Tanzania inabuni mbinu na mikakati mahsusi kwa lengo la kuwawezesha Diaspora kuendelea kuchangia zaidi katika maendeleo ya taifa kupitia maeneo ya kimkakati na kuwasihi wachangamkie fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zinazopatikana nyumbani.

Mhe. Pinda pia amewasihi Diaspora hao kutumia mifumo rasmi ya kutuma fedha nyumbani (remittances) ili kuiwezesha Serikali kuwa na taarifa na takwimu sahihi za mchango wa disapora kwa Taifa lao.

“Nichukue nafasi hii kuwajulisha kuwa Serikali iko katika hatua ya maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2050, niwasihi Diaspora mtumie ujuzi na uzoefu mlioupata huku ugenini kwa kutoa maoni yenu kwa ajili ya Dira ya mpya ya Maendeleo ya Mwaka 2050 kwani kwa kufanya hivyo mtaliwezesha Taifa kupata dira itakayolifikisha kule kunakotarajiwa, alisisitiza Mhe. Pinda.

Pia amewasihi Diaspora hao kuendelea kujisajili katika mfumo wa kidijitali ujulikanao kama Diaspora Digital Hub (DDH) ili kuiwezesha Serikali kuwa na takwimu sahihi za Diaspora wake na kufanikisha maamuzi ya kisera kwa kuzingatia idadi na mchango wa dispora kwa Taifa.

Mhe. Pinda amewaomba Disapora hao wa Botswana kuendelea kuitetea nchi yao, kudumudisha mila, desturi na tamaduni zao, kupendana, kusadiana, kuinuana na kutatua changamoto kwa pamoja huku wakiendelea kushirikiana na Balozi wao aliyepo Pretoria, Afrika Kusini kama mlezi wao na kufuata sheria za nchi mwenyeji na wakumbuke kuwa nyumbani kwao ni Tanzania.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa, Balozi wa Tanzania Afrika Kusini anayewakilisha pia nchi za Botswana na Lesotho Mhe. James Bwana; Balozi Dkt. Salim Omar Othman; Mwambata wa Biashara na Uwekezaji katika Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Bi. Happyness Godfrey pamoja na Watanzania wanaoishi nchini Botswana.

Maadhimisho hayo yalitanguliwa na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa ATB ambao uliambatana na Uchaguzi wa Viongozi wa ATB kwa Muhula mpya ambapo Bw. Naiman Kissasi alichaguliwa kuwa Mwenyekiti , Peace Byengozi alichaguliwa kuwa Katibu pamoja na Viongozi wengine wa Kamati Tendaji. Kupitia Maadhimisho hayo Benki ya CRDB pamoja na Kampuni ya KC LAND walipata fursa ya kunadi huduma zao mahususi kwa ajili ya Diaspora wa nchini Botswana.

Mhe. Pinda yuko nchini Botswana kwa ajili ya kuongoza misheni ya Uangalizi ya Uchaguzi. Mkuu wa Botswana ya SADC (SEOM) uliofanyika nchini humo tarehe 30 Oktoba, 2024 ambako Chama cha Upinzani cha UDC kilipata ushindi wa zaidi ya viti 31 vya Bunge la nchi hiyo na hivyo kukiondoa madarakani chama tawala cha BDP kilichokuwa kikiongozwa na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Mhe. Mokgweetsi Masisi .

Related Posts