Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema wanaendelea kumuhoji Mkurugenzi wa Dar24 Media, MacLean Mwaijoka pamoja na watu aliowataja kuna nao kwenye mazungumzo ya kibiashara wakati alipotoweka Oktoba 31, mwaka huu.
Mwajoka alitoweka Oktoba 31, 2024 na kupatikana Novemba 2, 2024 akiwa hai maeneo ya Buyuni, Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Jumatatu, Novemba 4, 2024, kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro amesema wanaendelea na uchunguzi, wanamuhoji Mwaijoka na watu aliowataja aliokuwa nao kwenye mazungumzo ya kibiashara.
“Jeshi la Polisi tunaendelea na upelelezi, tunamuhoji yeye mwenyewe Mwaijoka pamoja na hao watu aliowataja wakiwa kwenye mazungumzo ya kibiashara,” amesema Muliro.
Awali ilidaiwa Mwaijonga alipotea wakati akitoka ofisini kwao eneo la Rose Garden, Mikocheni jijini Dar es Salaam akiwa na gari yake aina ya Toyota Prado.
Wakati huohuo, Jeshi la Polisi kanda hiyo limesema limewakamata watu 47 kati ya hao 15 wakituhumiwa kwa wizi wa vifaa vya kuchimbia madini, 22 wakijihusisha na dawa za kulevya huku 10 wakituhumiwa na vitendo vya uvunjaji wa nyumba.
Kamanda Muliro amesema watuhumiwa hao wamekamatwa Oktoba 2024 wakijihusisha na vitendo mbalimbali vya kihalifu.
Amesema Oktoba 29, 2024 jeshi hilo liliwakamata watuhumiwa 15 kwa tuhuma za wizi wa kontena lililokuwa na vifaa mbalimbali vya kuchimbia madini, mali ya kampuni ya Mkuki ambavyo vilikuwa vinasafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Chunya mkoani Mbeya.
Amesema watuhumiwa 22 walikamatwa wakisafirisha, kuuza na kutumia dawa za kulevya, ikiwemo bangi huku wengine 10 wakijihusisha na uvunjaji wa nyumba mchana, usiku na kuiba.
“Kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kisheria, baadhi ya watuhumiwa walikamatwa siku za nyuma na baadaye kufikishwa mahakamani, wamepatikana na hatia, akiwemo Derick Kiyagoka, mkazi wa Kitunda amehukuniwa miaka 30 jela,” amesema Muliro.