Rufaa yawanusuru wawili waliohukumiwa kuwaua wanandoa

Arusha. Mahakama ya Rufani imewaachia huru wakazi wawili wa Mkoa wa Mara, waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kuwaua wanandoa.

Walioachiwa huru ni Mwita Magori na Nyamahonge Joseph ambao walihukumiwa adhabu hiyo baada ya kukutwa na hatia ya kuwaua wanandoa ambao ni Mgosi Chacha na Mtongori Mwita, kisha kuwaibia ng’ombe tisa.

Katika kesi ya msingi iliyosomwa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma Oktoba 15, 2020 iliwahukumu adhabu ya kifo Magori na Joseph, walioshitakiwa kwa

makosa mawili ya mauaji ya Chacha na Mwita, kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu.

Walidaiwa kuwaua wanandoa hao Mei 29, 2011 katika Kijiji cha Itununu wilayani Serengeti mkoani Mara na walitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kifo.

Hata hivyo, walikata rufaa Mahakama ya Rufani na kesi ikapewa namba 536 B ya mwaka 2020, wakipinga hukumu hiyo ya Mahakama Kuu.

Mahakama hiyo katika kikao chake kilichoketi Oktoba 30, 2024 Musoma kusikiliza rufaa hiyo, iliwaachia huru Magori na Joseph baada ya kushinda rufaa hiyo.

Hukumu hiyo ilitolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Shaban Lila, Panterine Kenye na Laila  Mgonya.

Kilichowanusuru ni ng’ombe waliodaiwa kukutwa nao ambao ndiyo kiini cha warufani hao kukamatwa na kufikishwa mahakamani na mauaji ya wenza hao, hazikuwasilishwa mahakamani kama ushahidi.

Katika hukumu hiyo, majaji hao walisema nyingine ni madoa ya damu kwenye panga na nguo za warufani hao, haikuthibitishwa kuwa ni damu ya binadamu (wenza waliofariki), ambapo utetezi wa warufani kuwa walikamatwa na nyamapori huenda ikawa ni kiini cha madoa ya damu.

Jaji Lila alisema kutokana na sababu hizo, Mahakama hiyo iliona upande wa mashitaka uliegemea kwenye tuhuma ambazo sheria haiwezi kuwatia hatiani.

Jaji Lila alisema wamepitia kwa uangalifu ushahidi wa pande zote mbili na inaonekana wazi hakukuwa na shahidi wa tukio la mauaji hayo, badala yake  warufani walishikiliwa na shahidi wa pili kabla ya Polisi kwenda kuwachukua na kuwapeleka kituoni.

Alisema upande wa mashitaka ulitegemea ushahidi wa shahidi wa pili kuwa waliwakamata warufani wakiwa na ng’ombe tisa walioibiwa kwenye zizi la wanandoa siku moja baada ya mauaji yao, hivyo  kuwahusisha warufani na mauaji hayo.

Alisema Joseph  na Magori, walidai kukamatwa na nyamapori kinyume cha sheria kwa kutega waya katika msitu wa Grumet na walikuwa wamempelekea shahidi huyo ili awatafutie wateja.

“Kwa kuzingatia matoleo haya yenye kutofautiana, suala muhimu Mahakama inayotaka lizingatiwe ni iwapo warufani walipatikana wakiwa na ng’ombe walioibiwa au la.”

“Kwa kuzingatia ukiukwaji wa utaratibu unaoonekana katika kesi, tunamlaumu Jaji kwa kuwaona warufani kuwa na hatia na kuwatia

hatiani, tunaruhusu rufaa na kufuta hukumu,” alisema Jaji Lila.

Katika kesi hiyo upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi watatu ambao ni Chacha Marwa, Johanes Chacha na Chacha Nyageko.

Shahidi wa kwanza ambaye kwa wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Manyara, alidai kupewa taarifa Mei 29,2011 kuwa Mwita ameuawa nyumbani kwake na alipoenda alikuta mwili wake una majeraha ya kukatwa mgongoni, shingoni, usoni na mkononi.

Alidai wakati huo, mke wa marehemu na mifugo haikuwepo nyumbani na walipopiga kelele kuita watu wengine kusaidia kumtafuta Chacha, wao waliendelea kumtafuta na walipofika umbali wa hatua 30, wakaukuta mwili wake.

Shahidi wa pili ambaye alitokea Kijiji cha  Kitunguruma, alidai Mei 30, 2011 saa mbili asubuhi, alipiga simu kuwajulisha kwamba  wamewakamata vijana wawili wakiwa na ng’ombe tisa.

Alidai walikutana na vijana hao wakiwa na panga lenye damu kwenye mpini na walikuwa wakiwaswaga ng’ombe tisa.

Alidai walipowahoji kwa nini mavazi yao yana damu, walidai kuna ng’ombe alikuwa amechoka asingeweza kutembea, hivyo walimchinja na kugawa nyama yake katika Kijiji cha Gethari.

Alidai walipowahoji zaidi watu hao kuhusiana na ng’ombe hao, walikiri kuwa wamewaiba Musoma Vijijini na wakaahidi kumpatia ng’ombe wawili ili awaachie waendelee na safari yao.

Hata hivyo, alidai kuwa aliwahadaa waingie chumbani kwake awahifadhi, lakini walipoingia alifunga mlango na baadaye alitoa taarifa Polisi waliofika kuwakamata watuhumiwa hao.

Shahidi wa tatu ambaye pia alikuwa eneo kulikokutwa miili hiyo, alidai wanandoa hao walikuwa na ng’ombe tisa na yeye alikuwa na uhusiano wa karibu na marehemu na alikuwa anajua alama walizowekewa ng’ombe hao.

Alidai Mei 28, 2011 alimtembelea marehemu kwa ushauri kwani alitaka kuuza ng’ombe mmoja na alibaini kwamba kulikuwa na ng’ombe tisa wenye alama CMKV, CMK, =, SS na wawili hawakuwa na alama yoyote.

Katika utetezi wake, Magori alidai kuwa walikuwa wakijihusisha na uwindaji haramu kwa kutumia waya wa kutega na siku hiyo walifanikiwa kumkamata mnyama wa porini na kwenda kwa shahidi wa pili wakiwa na nyama, kwa ajili ya kuwatafutia wanunuzi.

Alisema alimfahamu shahidi huyo tangu mwaka 2008 na alikuwa akimtafutia wateja wa nyama pori.

Alidai alishangaa siku hiyo badala ya kumpelekea wateja, aliwaita Polisi ambao waliwakamata kwa tuhuma za kuwaua wanandoa hao. “Kiukweli mimi sijaua mtu, nashangaa hii kesi imekujaje,” alidai Mwita.

Katika rufaa hiyo, Magori na Joseph walikuwa na sababu mbili ikiwemo Mahakama kukosea kisheria kuwatia hatiani na kuwahukumu adhabu ya kifo huku upande wa mashitaka ukishindwa kuthibitisha kesi yake.

Related Posts