Unguja. Ili kuboresha afya kupitia mpango wa ushirikiano wa Serikali na Sekta binafsi (PPP), Wizara ya Afya Zanzibar imeingia mkataba na Shirika la Marekani la Elektroniki Health Care Nework (EHN) kutekeleza maeneo makuu ya afya kisiwani humo.
Mkataba huo wa Dola za Marekani 373 milioni (Sh1.005 trilioni) utasaidia katika mafunzo, miundombinu na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kisiwani hapa.
Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo leo Jumatatu Novemba 4, 2024 wizarani hapo, Katibu Mkuu Wizara Afya, Dk Mngereza Miraji Mzee amesema mkataba huo unalenga kuhakikisha usalama wa afya na huduma za afya kwa Wazanzibari wote kuanzia tabaka la chini hadi la juu.
Amesema mkataba huo wenye maeneo makuu manne baada ya kuanza kutekelezwa na kukamilika, kwa kaisi kikubwa watakuwa wameboresha rasilimali watu madaktari na wafanyakazi wengine katika sekta ya afya kwa kupata elimu ya kisasa.
“Katika hili tutajenga Zanzibar Health Academy ambayo itatoa mafunzo ya kisasa kwa kutumia teknolojia ya kisasa na vifaa vya kisasa katika kuhudumia,” amesema.
Jambo lingine ni uboreshaji wa miundombinu katika kujenga hospitali na zahanati kuanzia ngazi ya chini hadi juu huku wakiangalia namna ya kuunganisha mifumo yote kwa kutumia mfumo wa ICT katika kuboresha utoaji wa huduma na kuondoa urasimu katika sekta ya afya.
Kuhusu muda wa utekelezaji wa mkataba huo, Dk Mngereza amesema utakuwa na hatua mbalimbali za utekelezaji.
“Kutaanza mambo ya ujenzi na kuweka mifumo ndani ya miaka mitatu iwe imekamilika na baada ya hapo utaanza ujenzi wa academy, lakini inategemewa ndani ya kipindi cha miaka mitano itakuwa mkataba umekamilishwa.”
Amesema baada ya kukamilika mkataba huo, lengo si kuhakikisha wananchi hususani wa hali ya chini wanapata sio tu huduma ya afya bali huduma bora za afya ambazo zinapatikana hata katika nchi nyingine.
“Baada ya hapo tunaingia katika utalii wa afya ambao watu wengine kutoka duniani waje Zanzibar kutibiwa na kutembea kama watalii,” amesema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa EHN, Jamal Bahabri amesema baada ya kusaini mkataba huo, wananchi wote katika kisiwa hicho wategemee kunufaika na mabadiliko makubwa katika sekta ya afya kwani wanakwenda kuleta utofauti.
“Makubaliano haya yanalenga kuchochea maendeleo ya utoaji wa huduma za Zanzibar afya na kupata huduma za kisasa kwa ngazi zote,” amesema.
EHN ni kampuni ya Amerika ambayo imebobea zaidi katika kukuza taasisi za huduma za afya, katika miundombinu na mifumo ya uendeshaji kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
“Tunaamini kwamba kila mmoja anastahili kupata huduma bora za afya na tunaaahidi kuchangia kufikia huko kujenga Zanzibar imara katika ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,” amesema na kuongeza;
“Tutajenga miundombinu ya afya, tutajenga misingi ya mwanga wa kesho familia zenye afya njema, na kuiwezesha jamii na tunaahidi kutoka moyoni na ni mpango wetu kuhudumia Wazanzibari katika safari hii kufikia afya bora,” amesema.
Mtaalamu huyo amesema watahakikisha wanatekeleza na kukamilisha yote waliyokubaliana kwenye mkataba kuisindikiza Serikali kufikia malengo yake ya kuwa na mifumo imara ya afya na wanaamini kwamba kuwekeza katika mifumo ya afya, kutachochea uchumi na kuwapa nguvu Wazanzibari.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya, Dk Amour Suleiman Amour amesema ni safari ya muda mrefu kuingia kwenye ushirikiano huo lakini wanashukuru wamefanikiwa na kwamba mkataba huo unazungumzia vipaumbele vya afya Zanzibar na uboreshaji wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kuipitia Bohari kuu Zanzibar.
“Watumishi watapata mafunzo katika ngazi ya jamii, kutakuwa na fedha zinaingizwa kwenye mfuko wa afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hata wale ambao hawana uwezo wa kulipia afya,” amesema.
Naye Kamishna wa Idara ya PPP, Emmanuel Mashimba amesema Serikali ilifungua dirisha la ushirikiano kwa lengo la kushirikiana na sekta binafsi kutoa huduma na mpango huo unaonesha mafanikio, kwani zipo huduma zimeanza kuimarika kupitia ushirikiano huo.
“Moja ya huduma hizo ni afya, kwa hiyo kampuni hii itawajibika kutoa huduma na kuwekeza miundombinu katika ushirikiano,” amesema.