Shule ya Msingi Fahari Elite kukuza vipaji vya michezo

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Shule ya Msingi Fahari Elite iliyopo Mvuti Dar es Salaam imesema imebuni programu mbalimbali kwa lengo la kuibua na kukuza vya michezo.

Akizungumza Novemba 2,2024 wakati wa bonanza lililofanyika shuleni hapo Meneja wa Shule ya Msingi Fahari Elite, Neema Mchau, amesema wanatumia mbinu mbalimbali kuibua na kukuza vipaji vya watoto kupitia michezo.

“Tuna wajibu mkubwa wa kuwasaidia watoto kuwianisha vipaji walivyonavyo na masomo. Tumeandaa bonanza kuwapa fursa watoto kuonyesha uwezo wao kwa sababu kipaji cha mtoto kikikuzwa kina nafasi kubwa ya kuamua mafanikio yake ya baadaye,” amesema Mchau.

Mgeni rasmi katika bonanza hilo ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Fahari, Christopher Chinyala, ameipongeza shule hiyo kwa kuandaa bonanza hilo ambalo litakuza vipaji vya michezo kwa watoto.

“Michezo inajenga afya na tukiwa na afya bora tunajenga uchumi ulio bora kwa kuwa tutaongeza ufanisi kazini,” amesema Chinyala.

Bonanza hilo limeshirikisha wanafunzi na wafanyakazi wa Shule ya Fahari Elite, Shule ya Msingi Mvuti, Robeli na timu ya soka ya Mchina FC kutoka Mvuti.

Michezo iliyochezwa ni soka, riadha, kukimbia na mayai, kufukuza kuku na kuvuta kamba ambapo washindi walokabidhiwa zawadi na vyeti vya ushiriki.

Related Posts