Japo katika baadhi ya maeneo miti hiyo imeshakatwa, lakini baadhi imebaki ikiwamo ya mjini Bagamoyo, Tabora, Ujiji, Morogoro na maeneo mengineyo.
Hii ni miti ya miembe iliyopangana barabarani na pengine kupandwa kwa ustadi mkubwa kama mtu aliyetumia kamba au rula.
Lakini unajua kama kuna uhusiano wa miti hiyo na biashara ya utumwa?
Simulizi za kihistoria zinaeleza kuwa miti hiyo ni kielelezo thabiti cha mapito au njia walizokuwa wakitumia watumwa kutoka mikoa ya bara kama vile Kigoma, Tabora, Morogoro kuelekea Bagamoyo na hatimaye Zanzibar kabla ya kusafirishwa nje.
Simulizi zinaeleza kuwa wafanyabiashara wa utumwa walikuwa wakipanda miembe hiyo kama ishara ya kuweka alama ya njia zao wakati wa kwenda kuchukua watumwa na kurudi, ndio maana kila walipopita kuna alama ya miti hiyo.
Kihistoria moja ya njia kubwa ya watumwa ilikuwa ni ile ya kuanzia Ujiji kuelekea Bagamoyo, ambapo hapo watumwa walipumzika kabla ya kwenda Zanzibar mahala kulipokuwa na soko kubwa la watumwa.
Hata hivyo, kwa Morogoro kuna simulizi nyingine kuhusu miti hiyo hasa ile iliyopo katika barabara ya kuelekea kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa na Ikulu ndogo, maarufu kama barabara ya Boma. Miembe hiyo imepandwa kulia na kushoto mwa barabara hiyo.
Sudi Kiroboto ni mzee na mzaliwa wa mtaa huo wa Boma, ameeleza historia ya miembe hiyo, akisema kuwa ilipandwa miaka ya 1800 na wakoloni wa Kijerumani, na lengo lao lilikuwa ni kuweka alama ya maeneo ya ofisi za serikali ya kikoloni.
“Hawa wakoloni waliweka alama hii ya miti kwenye kila mkoa na walikuwa walipanda kwenye zile barabara zinazoeleka kwenye ofisi zao kipindi hicho zilikuwa zinatambulika kwa jina la ‘bomani’. Ipo mikoa ambayo walipanda mibuyu na mikoa mingine walipanda miti waliyoona inafaa kuwa alama,’’ anasema na kuongeza:
‘’Sisi hapa Morogoro ndio ikapandwa miti ya miembe na kwa vile ilipandwa kwenye barabara hii ya kuelekea kwenye ofisi zao bomani, ndio maana hii barabara mpaka leo hii inaitwa ‘Boma road’.’’
Amesema kwa sasa miti hiyo ina umri wa zaidi ya miaka 200 ambapo zamani ilikuwa inazaa embe nyingi na tamu, lakini kwa sasa kutokana na kuzeeka, inazaa embe chache na hazina utamu ule uliokuwepo wakati huo huku mingine ikikoma kabisa kuzaa na kubakia kama miti ya vivuli tu.
“Zamani sisi tukiwa wadogo miembe hii ilikuwa sehemu ya michezo yetu maana embe zilikuwa zikidondoka zenyewe tena tamu kwelikweli, kipindi cha likizo, ukipita hapa muda wa asubuhi unakuta watoto wa mtaa huu wako barazani wanasubiri embe zianguke waokote, lakini kwa sasa unaweza ukakaa hata miezi mitatu usione embe ikianguka na hata hizo zinazoanguka ni zile ambazo tayari zimeshaoza mtini. Kwa sasa miembe hii tunafaidika nayo kwa kivuli tu na sio kula embe,” amesema Mzee Kiroboto.
Kiroboto ambaye pia ni mjumbe wa serikali ya Mtaa wa Boma, anasema faida iliyopo kwa miembe hiyo kwa sasa ni ndogo ukilinganisha na hasara, kwa kuwa tayari imeshazeeka na matawi yameanza kuoza na kudondoka kwenye paa za nyumba.
Naye Mkwembe Issa, amesema yeye ni mzaliwa na mji wa Morogoro katika kata ya Mbuyuni ambayo ni eneo jirani na barabara hiyo ya Boma.
Anasimulia kwamba alipokuwa mtoto mara zote yeye na rafiki zake walikuwa wakicheza kwenye miembe hiyo kwa ajili ya kuokota embe, lakini kwa sasa haizai kwa kiwango kile cha awali.
Ameshauri Serikali kutafuta namna ya kupunguza matawi ya miembe hiyo ama kuikata na kupanda miti mingine ambayo haitakuwa na madhara kwa wananchi.
“Kwa vile barabara hii imezoeleka kuonekana na miembe basi Serikali inaweza ikaamua kukata miembe hii iliyozeeka na kupanda mingine mipya ambayo haitakuwa na matawi makubwa ili alama hii iendelee kuwepo kama historia inavyoeleza. Kuendelea kuiacha miembe hii ni hatari maana matawi yake yanaweza kuleta madhara tawi linaweza likaangukia gari au mtu,” anasema Issa.
Juma Ng’ondavi ni mwenyeji wa mji wa Morogoro amesema miembe hiyo ilipandwa na Wajerumani kwenye maeneo yote waliyoishi. Na walipendelea miti yenye uwezo wa kuishi kwa miaka mingi kama miembe.
Ameshauri wakati huu ambapo Manispaa ya Morogoro iko kwenye harakati za kuwa jiji, ni vema miundombinu ya barabara ipanuliwe na hivyo barabara ya Boma ni moja ya barabara yenye umuhimu na inayopaswa kupanuliwa.
“Katika kupanua barabara hii ni lazima hii miembe iondolewe na kama ni alama ya kihistoria basi inaweza ikapandwa miti mingine ambayo haikuwi kwa kiasi hiki. Ipo miti ya aina nyingi ya urefu wa kupita nyumba, lakini kuiacha miti hii kutafanya hata majengo marefu yashindwe kujengwa,” anasema Ng’ondavi.