Katika mkutano wake wa Kampeni mjini Las Vegas Kamala Harris amemkosoa vikali Trump kwa maoni aliyoyaita “ya udhalilishaji mkubwa” kwa wanawake. Ameyasema hayo akiirejea kauli ya mpinzani wake huyo aliyesema katika mkutano wake wa Jumatano huko Green Bay Wisconsin kuwa atawalinda wanawake, “watake wasitake.”
Akiizungumzia kauli hiyo ya Trump, Harris amedai kuwa inawadhalilisha wanawake na ni kanakwamba hawaelewi mamlaka waliyonayo, haki na uwezo wa kufanya maamuzi kuhusu maisha yao binafsi ikiwemo miili yao.
Soma zaidi: Harris na Trump warushiana vijembe kwenye kampeni Wisconsin
Amesema ikiwa Rais huyo wa zamani atachaguliwa kuiongoza tena Marekani, atapiga marufuku utoaji mimba kote nchini humo, atazuia upatikanaji wa njia za uzazi wa mpango atahatarisha huduma za usaidizi zinazofahamika kama IVF. Haki ya uzazi imekuwa moja ya ajenda kuu za chama cha Democratic na kukipunguzia wafuasi chama cha Republican tangu wahafidhina walipochukua nafasi kubwa katika Mahakama ya juu ya Marekani na kuiharamisha haki ya uavyaji mimba mwaka 2022.
Trump aahidi kuikomboa Marekani Novemba 5
Kwa upande wake mgombea wa Republican Donald Trump akiwa mjini Henderson, amelizungumzia suala la uhamiaji na kuwaahidi wapiga kura kulikomboa taifa. Amesema Marekani ni taifa linalotawaliwa na kuwa Maelfu ya wahamiaji huingia nchini humo wakiwa na vifaa vyenye hadhi ya kijeshi. Amewaambia wapiga kura wake kuwa Novemba 5 mwaka 2024 itakuwa “siku ya ukombozi wa Marekani”.
Trump ameeleza kuwa kutokana na mipaka ya Marekani kuwa wazi, mpinzani wake ambaye ni makamu wa Rais, anasaidia kufanikisha ulanguzi wa binadamu, uingizwaji wa dawa za kulevya na kuingia kwa wafanya biashara hiyo haramu Marekani. Amedai kuwa walanguzi wa biashara haramu wana programu maalumu yenye namba ya simu wanayoweza kuipiga ili kupanga mahali pa kuwabwaga wahamiaji wasio na vibali.
Jimbo la Nevada walikofanya kampeni Harris na Trump ni moja ya majimbo saba yenye ushindani mkali kando ya Arizona, Georgia, North Carolina, Wisconsin, Pennsylvania na Michigan. Wawili hao wakiwa kusini magharibi wanajaribu kutafuta ushawishi wa wapiga kura wenye asili ya kilatino.
Haris na Trump wako pia kwenye harakati za kuwashawishi wapiga kura ambao bado hawajaamua wa kumchagua. Mahasimu hao wataelekea Milwaukee watakapofanya kampeni zao kwa nyakati zinazofanaana. Mji huo uko katika jimbo lenye ushindani mkali la Wisconsin.