Usiku wa Mbeya City wanoga

KLABU ya Mbeya City imeanzisha mpango mkakati wa kuhakikisha timu hiyo inarejea Ligi Kuu Bara msimu ujao kwa kuanzisha harambee inayoshirikisha wadau mbalimbali, itakayofanyika Novemba 6, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mkapa jijini Mbeya.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mbeya City, Ally Nnunduma alisema lengo kubwa la harambee hiyo ni kutoa nafasi kwa wadau wa Jiji la Mbeya kutoa maoni yao ambayo yatawasaidia kutimiza azma ya kukirejesha tena kikosi hicho katika Ligi Kuu Bara msimu ujao.

“Jiji la Mbeya bila ya Mbeya City haiwezekani, katika usiku huo zitauzwa bidhaa mbalimbali za timu na kama haitoshi pia tutaangalia namna bora ya kuhakikisha mashabiki wanasafiri katika michezo yetu ya ugenini iliyobaki msimu huu,” alisema.

Nnunduma aliongeza, licha ya mambo mbalimbali yatakayojadiliwa katika harambee hiyo, anawakaribisha wadau wote na wadhamini kujitokeza kwa ajili ya kukichangia kikosi hicho ili kiweze kurejesha heshima iliyojijengea hapa nchini.

Katika usiku huo wa Mbeya City mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera atakayeongoza harambee na wadau mbalimbali wa Jiji la Mbeya kuichangia timu hiyo, ipande tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023.

Related Posts