Dodoma. Wabunge wameitaka Serikali kujikita katika kuondoa umaskini wa mtu mmojammoja.
Mbali na hao, Mbunge wa Kuteuliwa (CCM), Shamsi Vuai Nahodha akisema na kutoa mifano ya baadhi ya matumizi ya Serikali ambayo badala ya kusaidia kuongeza tija yanaibebesha mzigo mkubwa.
Wabunge pia wameonyesha kukerwa kwa kuingizwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa miradi ya Liganga na Mchuchuma bila utekelezaji. Pia, wametaka kanuni za Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kuwekwa wazi kwa wabunge na Watanzania.
Wamesema hayo leo Jumatatu, Novemba 4, 2024 wakati Bunge lilivyokaa kama kamati kujadili na kushauri kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2025/26 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Akichangia hoja hizo, Nahodha amesema baadhi ya matumizi ya Serikali kwa maoni yake badala ya kusaidia kuongeza tija yanaibebesha mzigo mkubwa.
Ametoa mfano wa Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Maliasili ya Utalii, Wizara ya Maji wananunua mitambo inayofanana na wote wanafanya kazi ya kuchimba mabwawa na kutengeneza barabara.
“Baada ya muda mfupi tu, vifaa vinaanza kutelekezwa porini kwa sababu ya gharama za mafuta na matengenezo zimekuwa kubwa sana badala ya vifaa hivyo kuwekwa sehemu moja na kila anayehitaji kuvikodi,” amesema.
Ametoa mfano mwingine ni Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), kina shule nzima ya teknolojia ya habari, wakati huohuo Wizara ya Habari na Teknolojia ya Habari inajenga Chuo cha Umahiri cha Teknolojia na Tehama.
Nahodha aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali za Mapinduzi ya Zanzibar kuanzia mwaka 2000 hadi 2010, amesema hayo yote ni matumizi mabaya ya fedha.
“Sisi tatizo letu si majengo bali ni walimu walio bora, vifaa vilivyo bora na mazingira. Fedha ambazo zingetumika kujenga chuo kipya, zingepelekwa Udom ili kutengeneza chuo cha umahiri vijana wetu wapate mafunzo mazuri,” amesema Nahodha.
Amesema mfumo wa vyuo vikuu ambapo chuo kimoja kinafundisha kila somo bila kusisitiza umahiri na weledi, hayo ni matumizi mabaya ya raslimali za Taifa na kuwa ingekuwa vizuri kama wangegawa vyuo vikuu kulingana na weledi na ubobezi wa masomo.
“Udom kingefundisha masuala ya sayansi teknolojia na uvumbuzi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kingefundisha masomo ya sayansi ya jamii, Muhimbili kikaendelea kama kilivyo na Sua (Chuo Kikuu cha Sokoine), kikaendelea kama kilivyo,” amesema.
Aidha, amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ina dhamira ya kufundisha masomo ya ufundi na amali katika shule zote za sekondari sambamba na kuwa na vyuo vya Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (Veta) nchini, lakini uwezo haupo kutekeleza jambo hilo.
“Badala ya kutekeleza shule zetu za sekondari kufundisha masomo haya, ningependekeza tukawekeza kwenye ujenzi wa vyuo vya kisasa vya ufundi katika kila kanda,”amesema.
Amesema vyuo hivyo vipewe walimu mahiri katika ufundishaji na vifaa vya kutosha na masomo yatakayofundishwa yanayoendana na shughuli kuu za uchumi wa Tanzania kilimo, ufugaji, gesi asilia, madini, ujenzi na miundombinu.
Akosoa mbinu za kuondoa umaskini
Kwa upande wa umaskini, Nahodha amesema kama Tanzania inataka kupunguza umaskini miongoni mwa Watanzania, basi wawekeze wawekeze zaidi katika sekta ya kilimo.
Amesema wizara imekuwa ikitekeleza miradi miwili ambayo ni jenga kesho iliyo bora na ujenzi wa mabwawa 18 ya kilimo cha umwagiliaji maji.
“Nimezitafuta takwimu ili nione mradi wa kesho iliyo bora unavyoweza kutusaidia, kwa bahati mbaya mimi ni mjumbe wa kamati ya bajeti taarifa hizo sikuzipata,”amesema.
Kuhusu utekelezaji wa ujenzi mabwawa 18, Vuai amesema hadi sasa katika kipindi cha miaka mitatu, Wizara ya Kilimo imetekeleza ujenzi wa mabwawa matatu ambayo yamekamilika na 15 yapo katika hatua mbalimbali.
Amesema wangefanya hivyo, wangekuwa wamejenga mabwa 12 na mabwawa sita yaliyobaki, yangemalizwa mwaka ujao na kwa bahati mbaya wizara hiyo haikufanya hivyo.
“Licha ya wizara hii kupatiwa wastani wa Sh1 trilioni kila mwaka kwa ajili ya maendeleo ya kilimo, tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo bado iko chini sana,”amesema.
Amesema njia muafaka ya kuongeza tija katika uzalishaji iwe katika sekta ya kilimo au viwanda ni kuwekeza kwenye elimu bora inayosisitiza juu ya ufundi, ugunduzi.
Naye Mbunge wa Ludewa (CCM), Joseph Kamonga amesema pato la Taifa linakua vizuri lakini pato la mtu mmoja hata katika taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti bado wanaona ni changamoto.
Amesema endapo watawasaidia wakulima kupata soko la kutosha na ruzuku wanazopewa za mbolea pamoja na mbegu watazalisha zaidi kwa sababu watakuwa na uhakika wa soko.
Mbunge wa Kuteuliwa (CCM), Profesa Shukrani Manya amesema furaha ya Watanzania itakuwa mara dufu iwapo miradi ambayo imeendelea kuwa inatajwa mwaka hadi mwaka na yenyewe ikatekelezwa mapema kadri inavyowezekana.
“Mradi wa Kusindika na Kuchakata Gesi (LNG), ukikamilika au kuanza mapema ni kichocheo cha viwanda vya mbolea, kemikali kwa sasa tunaagiza mbolea nje ya nchi ingesaidia kuokoa fedha zinazotumika kuagiza bidhaa hiyo,”amesema.
Amesema mradi wa Liganga na Mchuchuma umekuwa ukitajwa mwaka hadi mwaka kwenye mipango na bajeti ya Serikali.
Ametaka katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka 2025/26, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo aseme ni lini miradi hiyo itakamilika, ili wasiendelee kupanga na kuhamisha katika mpango mingine inayokuja.
“Ninachoona kuna majadiliano yanachukua muda mrefu, tumeendelea kujadili bila kuweka ukomo, mimi ningetamani ili kupata manufaa ya miradi mikubwa inayoendelea vihatarishi viangaliwe, majadiliano yafupishwe ili ifikie mahali miradi hii ianze,”amesema Profesa Manya.
Kuhusu kubana matumizi fedha za uendeshaji, Profesa Manya alipendekeza mamlaka za maji zipewe tarrif maalumu ya umeme, ili kuwezesha wananchi wapate maji kwa gharama nafuu.
Mbunge wa Handeni Mjini (CCM) Rubein Kwagilwa amesema wakati wanajiandaa na kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote wapitie upya vyanzo vya mapato vya bima hiyo mbali ya vilivyopitishwa mwaka jana.
Amesema vyanzo vya mapato vilivyopitishwa mwaka jana hadi sasa wamekusanya Sh22 bilioni pekee yake kwenye lengo la kukusanya karibia Sh173 bilioni.
“Ni muhimu tukafanya tathimini na kuendelea kutafuta vyanzo vingine vya mapato kabla ya kuanza kutekeleza mwaka 2026. Na pia kuanzisha mfuko wa wasio na uwezo wa kugharamia bima ya afya kwa watoto, wajawazito,”amesema.
Amesema ni hatari fedha hizo kukaa katika mfuko mkuu wa Serikali badala yake iweke utaratibu wa kusimamia mfuko huo ambazo ni vyema zizalishe badala ya kuwekwa tu.
Amesema hatari inayoweza kujitokeza kwa fedha kuwekwa katika mfuko mkuu wa Serikali ni kutumika vinginevyo.
Kwagilwa ametaka kanuni za mfuko huo zifahamike kwa watu wote wakiwemo wabunge, waajiri kabla ya kuanza utekelezaji wa mpango huo.