WINGA wa Bunda Queens, Nelly Kache amesema kama mambo ya usajili hayatakamilika hadi dirisha dogo basi atarejea kwao Kenya.
Nyota huyo raia wa Kenya kabla ya kuitumikia Bunda alizichezea Alliance Girls (2023/24), Tiger Queens (2022/23) na Fountain Gate Princess (2021/22).
Hadi sasa Bunda kwenye michezo miwili ya Ligi iliwatumia wazawa kutokana na kushindwa kugharamia vibali kwa wachezaji wa kigeni.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kache alisema hadi sasa anafanya mazoezi na timu lakini hajacheza mechi yeyote jambo linalomfanya afikirie kurudi Kenya kwanza kusikilizia.
Kache aliongeza kuwa licha ya kutopata nafasi ya kucheza lakini mwenendo wa timu hiyo uko vizuri akiamini Bunda imekuja kuleta ushindani kwa klabu kubwa.
“Vibali imekuwa changamoto kubwa, nafikiria kama sitalipiwa hadi dirisha dogo nitarudi nyumbani kwa sababu siwezi kucheza, naamini yatashughulikiwa mapema na nitarudi uwanjani,” alisema Kache.
Kwenye mechi mbili ilizocheza Bunda Queens imeondoka na pointi mbili ikitoa sare ya 1-1 na Yanga Princess na JKT Queens ikiwa mkoani Mara.
Ukiachana na Simba, Yanga, Mashujaa Queens na JKT Queens, timu zilizosalia zote hadi sasa hazijakamilisha vibali vya wachezaji wa kigeni hivyo zimekuwa zikiwatumia wazawa tu.