WPL inarejea mechi nne zinapigwa

BAADA ya mapumziko ya siku 24 za kupisha kalenda ya FIFA kwenye michezo miwili ya kirafiki ambapo Twiga Stars ilicheza dhidi ya Morocco na Senegal, hatimaye ligi inarejea.

Hadi sasa zimechezwa raundi mbili za WPL, bingwa mtetezi Simba Queens akisalia kileleni baada ya kupata ushindi katika mechi zote ikifuatiwa na Mashujaa Queens yenye pointi nne sawa na JKT Queens iliyopo nafasi ya tatu.

Ligi inarejea kesho Jumanne zikipigwa mechi nne, Yanga Princess ikiwa nyumbani itaikaribisha Mashujaa kwenye Uwanja wa KMC, Get Program dhidi ya Bunda Queens, Ceasiaa Queens v Simba Queens na JKT Queens v Mlandizi iliyopo nafasi ya tisa kwenye msimamo baada ya kuambulia pointi moja.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa Yanga Princess, Edna Lema alisema wamepata muda wa kujiandaa na sasa wanarudi kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Mashujaa.

“Tunashukuru tumejiandaa vizuri na tutaanza na Mashujaa, moja ya timu nzuri. Naamini maandalizi yetu yatatupa ushindi ingawa haitakuwa rahisi,” alisema Lema.

Kocha wa Simba, Yussif Basigi alisema pamoja na kushinda michezo miwili akili yao kwa sasa ni kuwa na muendelezo mzuri ili kuhakikisha wanatetea taji hilo.

“Tunatamani kushinda kila mchezo na najua nina kikosi kizuri cha kunipa matokeo ingawa haitakuwa rahisi kutokana na ubora wa kila timu,” alisema Basigi.

Related Posts