Dodoma. Mkazi wa Mtaa wa Oysterbay Kata ya Dodoma Makulu jijini Dodoma Selina Jafar (30) amedaiwa kujifungua na kumuua mtoto kwa kumzamisha ndani ya ndoo ya maji akiwa chumbani.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi amekiri kufahamu tukio hilo akisema alipigiwa simu na wenye nyumba kujulishwa tukio hilo na alituma askari kufuatilia.
Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya majirani wamedai kuwa, tukio hilo limetokea jana Jumatatu Novemba 4, 2024.
Mmoja wa majirani hao, Mwamvita Madenge amesema alilala na mwanamke huyo nyumbani kwake baada ya kumwomba walale wote.
“Ilipofika saa 11 alfajiri alitoka nje nikamuuliza unakwenda wapi akanijibu kuwa narudi sasa hivi lakini alipotoka hakurudi tena aliingia chumbani kwake na kujifungia kwa ndani,” amesema Mwamvita.
Amesema mwanamke huyo ambaye anaishi peke yake alikuwa na tabia ya kulala mpaka saa saba mchana, lakini jana haikuwa hivyo alipitiliza mpaka majira ya saa moja usiku na kila walipokuwa wanamgongea alikuwa hataki kufungua.
Mwamvita amesema baada ya kuona kutakuwa na tatizo kutokana na ujauzito alionao, walimwita mwenye nyumba na kukubaliana wavunje mlango ili wajue kilichompata huko ndani kwa sababu vyumba vya jirani vilianza kusikia harufu ya uvundo kutoka kwenye chumba cha mwanamke huyo.
Mwamvita amesema walimwita mwenye nyumba ili azungumze na mwanamke huyo lakini alikataa na kumwambia aje kesho yake kwa sababu amechoka hawezi kuzungumza na mtu.
Baada ya kauli hiyo, amedai kuwa waliamua kuvunja mlango na kukuta amejifungua mtoto wa kike kisha kumuua na kumtumbukiza kwenye ndoo ndogo ya maji.
Mwenye nyumba Agness Machilo amesema alipovunja mlango na kuingia ndani alikutana harufu kali ya damu huku mwanamke huyo akiwa amelala kitandani anavuja damu bila msaada wowote na alipomuuliza kwa nini amejifungua bila kuita msaada kwa watu, alisema alikuwa anakojoa kwenye ndoo ndiyo akajifungua na mtoto akatumbukia kwenye ndoo akafa.
Amesema kutokana na hali iliyokuwamo kwenye chumba hicho walishindwa kutoa msaada wa haraka na ndipo walimpigia simu aliyekuwa balozi wa mtaa huo, Vick Kimzo aliyefika na kuwajulisha polisi tukio zima ambao walimchukua mwanamke huyo kisha kumwachia arudi nyumbani kwa ajili ya uangalizi wa karibu.
“Tulipofika polisi hali haikuwa nzuri kwa sababu alikuwa bado anatoka damu nyingi kwa hiyo nikaambiwa nimdhamini kisha nirudi naye nyumbani kwa ajili ya kumpatia huduma ya usafi na chakula na kisha leo nimrudishe tena polisi ili wafanye utaratibu wa kumpeleka Mirembe,” amesema Vick
Mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa kwenye chumba cha maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.