MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Adam Adam amesema anahitaji kupata utulivu mkubwa ili kubaki katika njia sahihi ya kuhakikisha msimu huu anakuwa na muendelezo wa kufunga kama alivyofanya msimu uliopita akiwa Mashujaa.
Msimu uliopita ndani ya Ligi Kuu Bara, Adam alimaliza na mabao saba, kitu anachokitamani kiwe na muendelezo na ikiwezekana azidi idadi hiyo na kuandika rekodi mpya katika ligi.
“Ligi kuwa ngumu ni kitu kizuri kinachoonyesha jinsi timu zilivyojipanga na soka kukua, kama mchezaji inanisaidia kuendelea kujituma bila kukata tamaa kwani bila kiwango natambua haitakuwa rahisi kufanya vizuri.
“Binafsi najitahidi kulinda utulivu wa akili ili nisitoke mchezoni na kuendelea kupambana kupata nafasi ya kucheza, itakayonifanya nitimize ndoto yangu ya kufunga mabao mengi,” alisema Adam ambaye msimu huu hajafunga bao.
Ndani ya Azam, mshambuliaji huyo ambaye ametua kikosini hapo msimu huu, amekuwa akisubiri mbele ya Nassor Saadun na Jhonier Blanco.
Kuhusu ushindani wa namba, Adam alisema: “Ushindani ni mkali, ila unanisaidia kutobweteka, kila mtu anapambana katika mazoezi kumshawishi kocha kupata nafasi ya kucheza, hilo linasaidia timu kuwa na kiwango kwani kila mchezaji anakuwa anatafuta namba.”