Auwa madai ya kufumaniwa na mke wa mtu

Geita. Faida Deus (34), Mkazi wa Bugalama Wilaya ya Geita ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake huku chanzo kikitajwa ni wivu wa mapenzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo akizungunza na waandishi wa habari leo Jumanne, Novemba 5, 2024 amesema marehemu alikatwa maeneo ya kichwani, utosini na kwenye mashavu majeraha yaliyosababisha kifo chake.

Kufuatia mauaji hayo, polisi mkoani humo linamshikilia Athuman Baseka (39) fundi seremala mkazi wa Kamhanga wilayani humo kwa tuhuma za kusababisha mauaji hayo.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, Oktoba 30, 2024 majira ya usiku marehemu akiwa chumbani na aliyekuwa mke wa Athuman walivamiwa na Athuman na kuanza kumshambulia na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake.

“Mtuhumiwa na mke wake walikuwa wamegombana na mkewe akaamua kurudi kwao, akiwa kwao alianzisha mahusiano na marehemu kitendo ambacho mumewe hakukubaliana nacho na ndipo siku hiyo aliamua kuja na kuwavamia,“ amesema Kamanda Jongo.

Waombolezaji wakiwa nyumbani kwa Faida Deus huko kata ya Bugalama Wilaya ya Geita.

Jongo amesema wivu wa mapenzi ni moja ya sababu kubwa za mauaji na kuwataka wannachi kutojichukulia sheria mkononi pindi wanapofumania kwakuwa hilo ni kosa la madai na wanaweza kulipwa fidia watakapofikisha kwenye vyombo vya sheria.

“Kama kuna mgogoro ni vizuri wakatoa taarifa kwenye vyombo vya sheria na sio kujichukulia sheria mkononi, kumfumania mtu ni kesi ya madai na unaruhusiwa kufungua kesi kudai fidia kama ulitoa ng’ombe 50 zitarejeshwa,” amesema Jongo.

Jesca Emanuel, mkazi wa Bugalama akisimulia maisha yake na mumewe wakati akiwa hai amedai waliishi na mumewe vizuri lakini toka Agosti mwaka huu alihama nyumbani na kudai amerudi kwa mama yake na hata alipokwenda ili wazungumze hakuwa tayari hadi alipopata taarifa kuwa amefumaniwa na mke wa mtu na kuuawa.

“Nikiwa nyumbani saa nane usiku huyo mke wake mwingine nasikia alikua amemuoa alipiga simu kwa kutumia simu ya mume wangu na kudai amevamiwa na jirani yangu alitoka na kukuta amevamiwa na kukatwa mapanga ndio wakamkimbiza hospitali lakini akipata matibabu alifariki dunia,” amesema Emanuel

Deus Masalu, baba wa marehemu amesema wakati wa uhai wake mtoto huyo alikua mpole asiependa ugomvi na kuiomba Serikali kumchukulia hatua mtuhumiwa huyo kwakuwa hata kama mwanae alikosea zipo njia za suluhu badala ya kujichukulia sheria mkononi.

Related Posts