DC Kibiti ataka vikundi utunzaji bahari vimulikwe

Kibiti. Mkuu wa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, Kanali Joseph Kolombo amewataka wataalamu wa mazingira kufanya tathmini ya misaada inayotolewa kuboresha mazingira ili kuona kama imeleta maendeleo.

Kanali Kolombo amesema hayo wilayani Kibiti jana Jumatatu, Novemba 4, 2024 alipokuwa akikabidhi hundi za mfano zenye thamani ya Sh106.7 milioni uliotolewa na Shirika la WWF kwa vikundi 10 vya kutunza mazingira ya bahari kutoka wilaya za Kibiti na Mafia, Mkoa wa Pwani na Kilwa mkoani  Lindi.

Kanali Kolombo amesema kutokana na wimbi la uharibifu wa mazingira, kumekuwa na mashirika yanayotoa misaada ya uboreshaji, hivyo wataalamu wa halmashauri wanapaswa kufanya tathmini na kuvisimamia vikundi vinavyopewa ruzuku.

“Mimi naomba tuangalie ni muda gani wameendelea kutoa misaada hii? Je, tukienda huko vijijiji tutavikuta vikundi? Hivyo kuna haja ya kufanya tathmini kupitia wataalamu, je hizo faida zinaonekana?”

Amewataka wataalamu wa halmashauri kunakotoka vikundi hivyo, kuvifuatilia ili misaada hiyo ilete tija.

“Tukivipa kazi na kuviachia halafu tukaenda kuangalia matokeo baada ya siku kadhaa, halafu tukaanza kulaani, sisi wataalamu tutakuwa hatujafanya kazi yetu vizuri.

“Unapovipa fedha, unavifuatiliaje hivi vikundi kuona vinakwenda vizuri. Bila kufanya tathmini wahisani watakuwa wanatuletea fedha nyingi lakini maendeleo hayaonekani,” amesema.

Mkuu wa Program ya Mambo ya Bahari (Marine) kutoka WWF, Dk Modesta Medard amesema fedha hizo zimewekwa moja kwa moja kwenye akaunti za vikundi.

“Hivi vikundi vinajikita katika kutunza mazingira kwenye vijiji vyao ikiwa pamoja na ufugaji wa nyuki, usimamizi wa rasilimali za vuvuvi, pia kuna Vicoba.

“Katika fedha hizo, Wilaya ya Kibiti ina vikundi viwili vinavyotapa Sh21 milioni, Kilwa inapata Sh43.7 milioni, Mafia Sh42 milioni ndio jumla inakuwa Sh106.7 milioni,” amesema.

Amesema pamoja na kutoa hizi fedha, wamepata pia vitendea kazi ikiwamo mizinga ya nyuki na vifaa vya kurina asali vya zaidi ya Sh30 milioni vitakavyopelekwa kwenye wilaya hizo.

“Kuna jumla ya vikundi 10 vyenye wanachama 230, kati yao wanawake ni 106 sawa na asilimia 46 na wanaume 124 sawa na asilimia 54 ya wanavikundi, kwa hiyo kunakuwa na uwiano wa wanawake na wanaume,” amesema.

Pia, amesema wanatarajia kuanzisha mashamba darasa kwa ajili ya kutolea mafunzo na kufanyia utafiti kwa wanafunzi wa shule za msingi hadi vyuo vikuu.

Ofisa Uvuvi wa Wilaya ya Kibiti, Mkuyange Manyama amesema kumekuwa na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi na shughuli za binadamu.  

“Wakati wa mafuriko hali inakuwa mbaya kwa sababu eneo lote linalopokea maji ya Mto Rufiji, kwa hiyo tope lote linaingia likipunguza kina cha bahari.

“Halafu kuna shughuli za kibinadamu, kwa mfano mifugo inayongia kwenye misitu inakanyaga mimea michanga,” amesema.

Ametaja pia kilimo, akisema wapo wanavijiji wanaolipa kwenye mikoko na kuikata ili wapate maeneo makubwa.

Akizungumzia msaada huo, Mwanasiha Khatib Mohamed kutoka kikundi cha Jitihada kilichopo Kijiji cha Jimbo wilayani Mafia, amesema wamepata mafunzo ya kutunza mazingira na fedha.

“Awali, tulikuwa hatujui kutunza mazingira wala kutunza fedha zitokanazo na miradi yetu, lakini sasa tumejifunza na tutaweza kutunza mazingira.

“Tunashukuru kwa kutupa ruzuku hizi zilizofika Sh13 milioni katika kikundi chetu, kwani sasa tutaweza kukamilisha shughuli zetu,” amesema.

Naye Erick Kapira mratibu wa Kikundi cha Mazingira ni Uhai Kilwa amesema ruzuku waliyopata itachochea utunzani wa mazingira ya bahari ikiwamo upandaji wa mikoko kwenye maeneo yaliyoathiriwa.

Related Posts