Mwanza. Kesi inayomkabili dereva wa Basi la Asante Rabi, Shedrack Swayi (37) anayedaiwa kusababisha ajali iliyoua watu tisa na kujeruhi 53 mkoani Mwanza imekwama kuendelea baada ya kuugua ghafla mahakamani.
Katika kesi hiyo ya trafiki namba 30855/2024, Swayi anakabiliwa na shtaka lenye makosa 64 kwa kuendesha gari kwa uzembe Oktoba 22, 2024 alipokuwa akiendesha Basi la Asante Rabi kwa kuligonga Basi la Nyehunge.
Mshtakiwa alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Oktoba 29, mwaka huu na kusomewa shtaka lenye makosa hayo ambayo alikiri kuyatenda mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Misungwi kinyume na Kifungu cha 41, 63 (2) (b) na 27 (1) cha Sheria ya Usalama Barabarani namba 168 marejeo ya mwaka 2002.
Leo Jumanne Novemba 5, 2024, mshtakiwa baada ya kupanda kizimbani Hakimu Mkuu Mkazi, Esther Maliki alimtaka Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Lilian Meli kuanza kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali (PH) ya shtaka linalomkabili.
Hata hivyo, hatua hiyo haikufanikiwa baada ya mshtakiwa (Shedrack) kunyanyua mkono kisha kuruhusiwa na hakimu kuzungumza ndipo akaeleza anajisikia vibaya (hayuko sawa kiafya).
“Mheshimiwa Hakimu, sijisikii vizuri kiafya,” alisema mshtakiwa huyo jambo lililomlazimu na hakimu huyo na kuahirisha shauri hilo hadi Novemba 11, mwaka huu kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
“Kwa kuwa mshtakiwa ameomba kuwa hali yake kiafya siyo nzuri basi tunaahirisha shauri hili hadi tarehe 11 Novemba 2024,” amesema Hakimu Meli.
Wakati huo, mshtakiwa ameachiwa kwa dhamana baada ya kukidhi masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili wenye Kitambulisho cha Taifa (Nida) waliosaini bondi ya maneno ya Sh5 milioni kila mmoja.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Shedrack anakabiliwa na shtaka lenye makosa 64 ikiwamo kuendesha gari kwa uzembe katika barabara ya umma na kusababisha vifo vya watu tisa, majeruhi 53 na uharibifu wa mali.