BAADA ya Fox Divas ya Mara kushindwa kufuzu kucheza mashindano ya ubingwa wa Afrika (AWBL), Mkurugenzi mtendaji wa timu hiyo, Aloyce Renatus amesema hasira zao kwa sasa wamezielekeza katika Ligi ya Taifa (NBL).
Mashindano hayo ya kufuzu yalifanyika mjini Zanzibar na Eli-hillay ya Misri na Reg ya Rwanda ndizo zilizofuzu mashindano hayo.
Timu hizo zitaungana na zilizoshinda katika kanda zingine, kwenye mashindano ya ubingwa wa Afrika (AWBL) yatakayofanyika Senegali, Novemba mwaka huu.
Renatus alilimbia Mwanaspoti, baada ya kutofuzu mashindano hayo, waliingia kambini moja kwa moja Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya Ligi ya Taifa ya Kikapu (NBL).
Akiongea kwa kujiamini, alisema kupitia mashindano ya Zanzibar walijifunza vitu vingi vya kiufundi uwanjani, hali iliyofanya uwezo wao wa kiuchezaji uongezeke.
Mashindano ya NBL yatafanyika katika viwanja vya Chinangali, Dodoma Novemba mwaka huu na bingwa mtetezi wa mashindano hayo kwa upande wanawake ni Vijana Queens na upande wanaume ni JKT.