KINARA wa mabao Ligi Kuu Bara, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ amebeba matumani ya Fountain Gate leo Jumanne ambapo watakuwa nyumbani, Tanzanite Kwaraa kuwakaribisha Pamba Jiji ambao bado wanajitafuta.
Fountain Gate yenye pointi 17 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikishika nafasi ya tano, chini ya Kocha Mohamed Muya, imeonyesha kuwa na mwenendo mzuri tofauti na wapinzani wao, Pamba Jiji ambao wapo nafasi ya 15 wakikusanya pointi tano, bado hawajaonja ushindi wa mechi za Ligi Kuu Bara.
Katika mechi tano za mwisho, Fountain Gate imeshinda michezo miwili dhidi ya Kagera Sugar (1-0) na KMC (3-1), lakini ikapoteza mbele ya Singida Black Stars (2-0) na Tanzania Prisons (3-2), na kutoka sare dhidi ya Mashujaa kwa mabao 2-2.
Kwa upande wa Pamba Jiji, timu hiyo inayoongozwa na Kocha Fred Felix Minziro imetoka sare mara moja dhidi ya Kagera Sugar (1-1) huku ikipoteza michezo minne dhidi ya Namungo (1-0), Tabora United (1-0), Yanga (4-0) na Coastal Union (2-0).
Hali hii inaweka shinikizo kwa Minziro na kikosi chake kutafuta matokeo mazuri ili kuinua morali ya timu.
Fountain Gate inajivunia Gomez, ambaye ni kinara wa mabao akiwa nayo sita msimu huu. Mbali na Gomez, kuna William Edgar na Salum Kihimbwa ambao pia wanachangia sana kwenye ushambuliaji wa timu hii, huku Kihimbwa akiwa na mabao matatu na asisti nne.
Mshambuliaji huyu ameonyesha uwezo mzuri wa kusaidia na kufunga, jambo ambalo linatoa changamoto kwa safu ya ulinzi ya Pamba Jiji.
Kwa upande wa Pamba Jiji, Kocha Minziro ana silaha muhimu kwenye safu ya ushambuliaji kupitia George Mpole, mshambuliaji aliyewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2021/22. Ingawa Pamba Jiji haijafanikiwa kupata ushindi msimu huu, uwepo wa Mpole unaweza kuwa na athari kubwa iwapo atapata nafasi nzuri za kufunga dhidi ya Fountain Gate.
Kocha wa Fountain Gate, Mohamed Muya alisema: “Mchezo huu ni muhimu sana kwetu. Tumekuwa tukifanya kazi kwa bidii kwenye mazoezi, na nina imani kwamba tutapata matokeo mazuri. Tuna timu yenye uwezo na kila mchezaji ana nafasi yake ya kufanya vizuri. Ni wakati wetu kuonyesha kile tunachoweza.”
Kwa upande wake, Fred Felix Minziro, alisema: “Bado hatujapata ushindi kwenye ligi, lakini hatupaswi kukata tamaa. Kila mchezo ni fursa ya kujifunza na kuboresha. Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya kuingia kwenye mchezo huu na mtazamo chanya. Lengo letu ni kupata ushindi.”