Hii hapa sababu ya Kapombe na Tshabalala kubaki Simba

KWA muda mrefu, Simba SC imekuwa ikiimarisha kikosi chake katika vipindi tofauti vya usajili. Maboresho hayo huwa yanagusa maeneo yote ya uwanja kuanzia golikipa, mabeki, viungo na washambuliaji.

Mwanzoni mwa msimu huu, Simba ilifanya usajili wa wachezaji 15 ambapo waligusa maeneo yote, kisha baadaye wakamuongeza mwingine.

Golini wamemuongeza Moussa Camara ambaye amekuja kuungana na Ally Salim, Ayoub Lakred na Aishi Manula. Kisha beki wa kulia akasajiliwa Kelvin Kijili, kumbuka upande huo yupo Shomari Kapombe na David Kameta ‘Duchu’.

Beki wa kushoto ambapo kwa muda mrefu anacheza Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ameletwa Valentine Nouma, lakini pale kati wakaongezwa Abdulrazack Hamza na Chamou Karaboue ambao wanaungana na Che Malone Fondoh na Hussein Kazi.

KS01
KS01

Kiungo cha ukabaji kuna Fabrice Ngoma, Mzamiru Yassin akaongezwa Yusuph Kagoma, Debora Fernandes na Augustine Okejepha.

Mbali na hao, wengine walioongezwa ni Omary Omary (kiungo), Joshua Mutale (winga), Awesu Awesu (kiungo mshambuliaji), Jean Charles Ahoua (kiungo mshambuliaji), Leonel Ateba (mshambuliaji), Valentino Mashaka (mshambuliaji), Steven Mukwala (mshambuliaji) na winga Elie Mpanzu aliyetua wakati tayari usajili umefungwa na anatarajiwa kuanza kuichezea timu hiyo pindi dirisha dogo likifunguliwa Desemba mwaka huu.

Ukiangalia katika marekebisho yote hayo ya kikosi, Tshabalala na Kapombe ndiyo wachezaji ambao wamekuwa hapo kwa muda mrefu na wanaendelea kucheza kikosi cha kwanza kulinganisha na wengine.

Uzoefu na kujituma kwa wachezaji hao ndiyo kitu kikubwa ambacho kinawabeba mabeki hao tegemeo ndani ya kikosi cha Simba.

Lakini pia, kucheza kutokana na maelekezo ya mwalimu sambamba na kile ambacho beki wa kisasa anahitaji kuwa nacho, nayo ni silaha nyingine kwa nyota hao.

KS02
KS02

Tshabalala ambaye ameitumikia Simba huu ukiwa ni mwaka wa 10 mfululizo yupo hapo, awali alianza taratibu ambapo wakati anatua mwanzoni mwa msimu wa 2014/15 akitokea Kagera Sugar, alimkuta Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ akapambania naye namba.

Alipoondoka Baba Ubaya, namba hiyo ikawa ni kama yake licha ya kwamba amekuwa akiletewa washindani tofauti kila mara, lakini anawashinda.

Katika usajili wa dirisha dogo msimu wa 2017/18, Simba ilimsajili Asante Kwasi kutoka Lipuli, alimpa changamoto Tshabalala lakini akaishinda vita mpaka leo hii amekuja Nouma ambaye bado hajafanikiwa kutoa ushindani. Hapo kati alikuwepo Gadiel Michael naye hakutoboa.

Takwimu za Ligi Kuu Bara msimu huu zinaonyesha Tshabalala amecheza mechi zote nane, kati ya hizo sita akimaliza dakika zote tisini, moja dhidi ya Prisons alifanyiwa mabadiliko kisha dhidi ya Namungo aliingia kutokea benchi.

Tshabalala ambaye ni nahodha wa Simba, anabebwa na vitu vingi vinavyowafanya makocha mbalimbali wanaokuja kuifundisha Simba kuendelea kumuamini.

KS03
KS03

Ukiachana na uzoefu alionao, lakini pia ni mzuri katika kutengeneza masbambulizi na kulinda lango lao.

Katika ligi msimu huu, amefanikiwa kuhusika kwenye mabao matatu akitoa asisti mbili na kufunga moja.

Majeraha ndiyo kitu ambacho kinamuangusha Kapombe, lakini anapokuwa fiti, hakuna kocha wa Simba aliyethubutu kumuweka benchi.

Hata wakati ambao aliachwa kwenye kikosi cha Taifa Stars sambamba na Tshabalala, nguvu ya Watanzania kuulizia sababu za kukosekana kwao zikawafanya kurejeshwa na kwenda Ivory Coast kushiriki michuano ya Afcon 2023.

KS04
KS04

Kapombe ambaye hivi sasa anaitumikia Simba kwa Kipindi cha pili, awali alikuwa hapo 2011 hadi 2013, kisha akarejea 2017 ambapo yupo hadi sasa.

Changamoto ya majeraha yaliwahi kuhatarisha uwepo wake ndani ya Simba hasa msimu wa 2018/19 ambapo alikuja Zana Coulibaly kumsaidia.

Lakini baada ya hapo, Kapombe amekuwa mchezaji muhimu wa Simba katika beki wa kulia akiendelea kutoa somo kwa Duchu na Kijili.

Kapombe naye ni kama Tshabalala linapokuja jukumu la kuzuia analifanya vizuri, lakini pia katika ushambuliaji anasaidia. Akiwa na bao moja katika Ligi Kuu Bara, pia amefanikiwa kutoa asisti moja.

KS05
KS05

Kwa wanachokifanya Kapombe na Tshabalala ndani ya Simba dhidi ya wale wanaoshindana nao, kinawapa nafasi ya moja kwa moja kucheza kikosi cha kwanza.

Kijili ambaye anasifika kuwa na mbio, sio mzuri katika kukaba lakini anapofika kwenye eneo la mwisho la kushambulia hana utulivu, huku mwenzake Duchu akikosa vyote hivyo – kukaba na kusaidia mashambulizi sio mzuri.

Nouma ambaye tumemuona kwenye mechi mbili za ligi dhidi ya Dodoma Jiji aliyotokea benchi na ile ya Namungo aliyoanza anaonekana sio mzuri sana katika kuwahi eneo la kuzuia pindi anapokwenda kusaidia mashambulizi.

Katika hilo, Tshabalala amekuwa akifanya vizuri kupandisha mashambulizi na kurudia haraka kukaba pindi wanapopoteza mpira kitu ambacho kinambeba zaidi.

Kwa mujibu wa majarida ya ufundishaji wa mpira wa miguu kama inavyosisitizwa katika taaluma hiyo, beki wa pembeni anatakiwa kuwa na uwezo wa kupokonya mipira kwa kuserereka (tackling).

KS06
KS06

Pande zote kushoto na kulia anapaswa kuwa na uwezo mkubwa wa kukaba awe na uwezo mzuri wa kupiga vichwa kutoka pande zote anapaswa kuwa na mahesabu ya uhakika anapokuwa anamkabili adui anayekuja na mpira wa miguu.

Pia anapaswa kuwa mwepesi katika kuingilia kati pasi (interception), anatakiwa kuwa na uwezo wa kutoa pasi fupi na ndefu, pia awe na uwezo wa kupanda kusaidia mashambulizi na awe mwepesi kurudi katika nafasi yake anatakiwa kuwa mwepesi na fundi mzuri wa soka.

Hizi ni baadhi ya sifa zinazohitajika kwa mabeki wa pembeni na wanapozikosa hawapaswi kufikiriwa kupangwa katika nafasi hiyo.

Miongoni mwa sifa alizonazo Tshabalala na Kapombe ni uwezo wa kumilliki mpira (ball control) kupandisha mashambulizi, uwezo wa kupiga pasi fupi na ndefu na krosi safi.

Mabeki hao pia wana uwezo mzuri wa kunyang’anya mipira – kwa hakika ni mabeki mzuri kwa wakati huu.

MSIKIE TSHABALALA ANACHOKISEMA

Tshabalala anasema sio rahisi kutumika ndani ya timu moja kwa muda mrefu na kuendelea kuaminika kama wengi wanavyodhani, bali kwa upande wake amepitia changamoto nyingi lakini imekuwa ni kama sehemu ya kujifunza.

“Kitu pekee kimeweza kunifanya nisalie Simba licha ya changamoto zote nilizowahi kupitia ni kusimamia malengo niliyonayo, kwa sababu mpira ndio kazi yangu ninayoitegemea kuniendeshea maisha, hivyo lazima nihakikishe hiki ninachokifanya nakifanya kwa ubora ili niweze kufanikiwa.

“Lakini pia, kila wakati nimekuwa mtu ambaye ninahakikisha napita kwenye misingi ambayo mpira unahitaji, hivyo nimekubali kufuata misingi ya soka na sio hiyo misingi inifuate mimi, hivyo siku zote nimekuwa mwanafunzi wa soka ili nijifunze zaidi na kubaki kwenye mstari,” anasema Tshabalala na kuongeza:

“Ukiangalia nafasi ninayoicheza mnaweza kuwa zaidi ya watu sita, kwa hiyo unapoipoteza nafasi unaweza usiwe bora zaidi na kikubwa ni kupambania kupata namba na kuhakikisha kwamba unafanya vizuri kila leo.

“Urahisi wa kuwapangua mabeki wengi ninaupata kwa sababu mimi ndio nipo hapa siku zote kama mwenyeji, hivyo mtu anayekuja kwako lazima kwanza akuangalie wewe unafanya nini na hata kocha anapokuja lazima akupe nafasi mwenye uzoefu. Kwa hiyo ukizingua ndio nafasi inakwenda kwa mwenzako ndio maana ninahakikisha sipotezi nafasi yangu.”

Related Posts