Sengerema. Kikongwe Chem Mayala (91), mkazi wa Kijiji cha Nyamazugo wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza amesimulia machungu aliyopata kwa kufiwa na mumewe Masasila Kibuta (102), siku 60 baada ya kufunga ndoa, akisema katika kipindi hicho kifupi waliishi kwa upendo na amani.
Chem aliolewa na Kibuta baada ya mkewe wa kwanza kufariki dunia na waliishi kinyumba kwa miaka mingi na kufanikiwa kuzaa watoto 10.
Ndoa hiyo ilifungwa Juni 17, 2023 mbele ya Padri Julian Mondula wa Parokia ya Ngomamtimba Jimbo Katoliki Geita, lakini baada ya siku 60 tu yaani Agosti 18, 2023 Kibuta alifariki dunia.
Akizungumza na mwandishi wa Mwananchi aliyemtembelea nyumbani kwake Nyamazugo Sengerema leo Jumanne Novemba 5, 2024, Chem amesema tangu mwaka jana amejikuta kwenye upweke mkubwa.
“Namkumbuka sana, ameniachia upweke, licha ya kuwa na umri mkubwa tulikuwa tukiishi kwa upendo. Hivi sasa ninaishi peke yangu, imani pekee niliyonayo ni kuwa ipo siku tutakutana na kuendeleza upendo wetu,” amesema kikongwe huyo.
Chem amesema ndoa yao ilikuwa na mvuto wa kipekee kutokana na umri waliokuwa nao.
“Ile ilionyesha ni kwa namna gani tulikuwa tunapendana na kutimiza kusudi la Mungu tukiwa wakongwe,”amesema Chem.
Amesema akizidi kumkumbuka mumewe na kulemewa na maumivu, huwa anakwenda kusali kwenye karibu lake.
“Ninaposali namuombea, nikifanya hivyo napata faraja, naiomba jamii kuwaombea watu waliotangulia mbele ya haki na kufanya usafi kwenye nyumba zao za milele ili wapate thawabu mbinguni,”amesema Chem.
Ndoa ya vikongwe hao ilikuwa gumzo ndani na nje ya Wilaya ya Sengerema.
Mtoto wa marehemu Masasila, Maria ambaye kwa sasa anamlea mama yake, anaiomba Serikali imuunge kwenye mpango wa kunusuru Kaya masikini unaoendeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) ili apate fedha zitakazomsaidia kutokana na ukata uliopo kwenye familia yao.
“Kwa sasa mimi ndiyo ninamlea mama yetu ndugu wengine wamesambaa maeneo mbalimbali wakiishi na familia zao, kutokana na kupanda kwa gharama za maisha nahitaji msaada,” amesema Maria.
Felesian Amos ambaye ni mjukuu wa Chem amesema wanapopata nafasi huwa wanakwenda kumsaidia bibi yao kwenye shughuli za kilimo.
Robert Malehe, jirani ya kikongwe Chem, amesema licha ya mzee Masasila Kibuta kufariki dunia bado wana uhusiano mzuri na familia hiyo kutokana na kikongwe huyo kuwatembelea na kuzungumza nao.
“Huwa anatutembelea na sisi tunafanya hivyo pia, kwa kweli tunausifu utukufu wa Mungu kuwa na bibi mwenye umri mkubwa lakini anayeweza kutembea na kutambua kila anachokifanya,” amesema Malehe.
Akizungumza na Mwananchi Juni 2023 katika mahojiano maalumu nyumbani kwake kuhusu ndoa yao, Mzee Kibuta mwenye watoto 10, alisema kwa kipindi kirefu, familia yake haijakutana pamoja na amekuwa akitafuta fursa ya kuikutanisha kwa kuitisha vikao bila mafanikio.
“Mimi na mke wangu Chem tumejaaliwa kupata watoto 10 na tunao wajukuu 86 na vitukuu 50, lakini kwa kipindi kirefu hatujawahi kukutana uso kwa uso kama familia; jambo ambalo lilikuwa likitunyima amani kwa sababu hata tukiitisha vikao wana familia wote hawafiki,” anasema Mzee Kibuta.
Alisema lengo la kubariki ndoa yao ni kujenga maisha yake kiroho na kuwakutanisha ndugu.
“Pamoja na kutengeneza maisha yangu ya kiroho ili nikifa ninakutane na Mungu, uamuzi wa kufunga ndoa katika umri mkubwa pia unalenga kuikutanisha familia pamoja kwa kuwa imetawanyika na haijakaa pamoja kwa kipindi kirefu,” alisema.