MSHAMBULIAJI wa zamani wa Azam FC, ambaye kwa sasa anakipiga MC Alger, Kipre JR amewaambia wenzie kwamba Stephane Aziz Ki na Prince Dube kuwa ndio wachezaji wa kuchungwa ili wasiwaadhibu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambako watakutana baada ya kupangwa kundi moja na Yanga.
Yanga ipo kundi A sambamba na MC Alger, Al Hilal na TP Mazembe, na mchezo wao wa kwanza wanatarajia kuanzia uwanja wa nyumbani dhidi ya Al Hilal kati ya Novemba 26 au 27 mwaka huu.
Kipre Jr ambaye ameondoka nchini mwishoni mwa msimu uliopita akiacha rekodi ya kuwa kinara wa asisti (9) ameliambia Mwanaspoti kuwa anafurahi kurudi Tanzania na kukutana na wachezaji anaowafahamu lakini watajipanga vilivyo.
Alisema anaifahamu Yanga ni timu bora na ina wachezaji wengi wazuri hivyo hawatarajii mteremko kutoka kwao wana kazi kubwa ya kufanya ili kupata matokeo dhidi ya timu hiyo na tayari wameanza mikakati.
“Yanga ni timu nzuri imekamilika kila eneo,. lakini Aziz Ki na Dube ndio wachezaji wa kuchungwa sana kwasababu nawafahamu ni bora ukiwaacha kidogo wanakuadhibu,” alisema na kuongeza;
“Dube namfahamu vizuri nimecheza naye Azam FC ni mshambuliaji mzuri na kwa upande wa Aziz Ki kila mmoja anafahamu ubora wake, msimu ulioisha nikiwa Azam FC aliibuka mfungaji bora. Ni aina ya mchezaji ambaye asipokufunga basi atamtengenezea mtu afunge.”
Kipre JR ambaye msimu huu amecheza mechi nane za ligi na hajafunga lakini akitupia bao moja kwenye Ligi ya Mabingwa hatua ya awali, ameliambia Mwanaspoti kuwa kwa upande wake sio mgeni kwenye mchezo wao na Yanga lakini anatarajia ushindani mkubwa.
“Yanga ina wachezaji wengi wazuri na wazoefu wa mashindano ya kimataifa, hawawezi kutupa mchezo mwepesi, nafikiri sisi pia ni bora na ndio maana tumefika nafasi hii tuliyopo sasa, baada ya droo kumekuwa na maneno mengi hata ndani ya klabu wamekiri kuwa wamewahi kukutana na timu hiyo japo ni muda mrefu,” alisema na kuongeza;
“Baada ya droo Yanga ilipopangwa kundi moja na sisi viongozi walisema wanaifahamu timu hiyo na wameshawahi kukutana nayo, nafikiri kwa muda waliokutana na timu hiyo kuna mabadiliko makubwa na mimi niliizungumzia ni timu ya aina gani.”
Kipre JR alisema amefurahi kupangwa kundi moja na timu ambayo anaifahamu na anatarajia kukutana na wachezaji wengi ambao wamecheza ligi moja hivyo, atajipanga kuhakikisha anaonyesha ubora kwa lengo la kuipambania timu yake ivuke hatua inayofuata.
Mshambuliaji huyo kabla ya kutimka Azam FC msimu uliopita alifunga mabao tisa na kuasisti tisa vilevile, aliuzwa na matajiri wa jiji la Dar es Salaam baada ya kuitumikia timu hiyo kwa misimu miwili alipojiunga nayo akitokea Sol FC ya Ivory Coast kwa mkataba wa miaka mitatu.
Kabla ya kutua Azam FC alishawahi kuitumikia Asec Mimosas, 2018-2020 ubora wake ulimfanya apate nafasi ya kuitumikia timu ya taifa ya vijana ya Ivory Coast U-15 na U-17, pamoja na kikosi cha wachezaji wa ndani (CHAN) 2020.
Msimu wake wa kwanza ndani ya kikosi cha Azam FC haukuwa mzuri kwake kwani alifunga mabao mawili tu na kutoa asisti nne lakini msimu wake wa pili ndio ulikuwa bora akishirikiana na Feisal Salum ‘Fei Toto’ waliipambania timu hiyo kumaliza nafasi ya pili na kufuzu Ligi ya Mabingwa.