Mbaroni wakituhumiwa kumuua mfanyabiashara wa madini Chunya

Mbeya. Jeshi la Polisi linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Peter Bruno (59), kwa kupigwa risasi akiwa nyumbani kwake, Oktoba 12, mwaka huu.

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne, Novemba 5, 2024, amesema Bruno alipigwa risasi mgongoni akiwa nyumbani kwake, Kata ya Matundasi, wilayani Chunya mkoani Mbeya.

Ameeleza kuw,  tukio hilo lilitokea saa 2:00 usiku na kwamba, watuhumiwa watatu wanaoshikiliwa walidaiwa kumvamia nyumbani kwake na baada ya mauaji walitokomea kusikojulikana.

 Hata hivyo, amesema watuhumiwa hao walikamatwa Novemba mosi, 2024.

“Baada ya tukio hilo, polisi walianza ufuatiliaji chini ya mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa na Novemba mosi, watuhumiwa walitiwa nguvuni wakiwa katika Kata ya Ubaruku wilayani Mbarali walikokimbilia,” amesema Kamanda Kuzaga.

Amesema wanaoshikiliwa ni Kenedy Richard (26), maarufu kama Maji Ulaya, mkazi wa Kijiji cha Garura, Wilaya ya Songwe, Msafiri Peter (48), maarufu kama Wakwetu, mkazi wa Matundasi, wilayani Chunya na Uhuru Sukwa (63), mkazi wa Magamba wilayani Mbozi, Mkoa wa Songwe.

Amesema baada ya kuwahoji, watuhumiwa hao walikiri kuhusika na mauaji hayo na walikutwa na silaha iliyotumika.

Wakati huohuo, Kamanda Kuzaga amesema mkazi wa Kata ya Forest Mpya, Hamza Shizya (50) anashikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya mke wake, Emmy Mwasile (35) kisa kikidaiwa ni kuwa na uhusiano nje ya ndoa.

Amesema tukio hilo lililotokea Oktoba 20, 2024, mtuhumiwa alimpiga marehemu kwa kitu kizito sehemu mbalimbali za mwili wake na  kumsababishia kifo.

“Mtuhumiwa alitoroka baada ya mauaji hayo na Oktoba 23 saa tisa alasiri, alikamatwa katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Tunduma akiwa katika jaribio la kuvuka mpaka kuingia Zambia,” amedai Kamanda Kuzaga.

Amesema uchunguzi unaendelea na utakapokamilika atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Related Posts