Mume, mke wasioona wasimulia wanavyoendesha maisha yao

Mbeya. Licha ya changamoto wanazopitia, wanandoa Upendo Tebela na mumewe Andindilile Mwakifumbwa wanaendelea kuishi kwa matumaini, wakiwa na imani kuwa kesho yao itakuwa bora zaidi.

Wawili hao wamekuwa wakiishi na ulemavu wa macho tangu utotoni na wamefanikiwa kuwa na mtoto mmoja wa kiume aitwaye Agape Andindilile (2).

Mwananchi ilifika nyumbani kwao Mtaa wa Mbalizi 2, Wilaya ya Mbeya Vijijini na kuzungumza na wanandoa hao wakieleza furaha na changamoto wanazokutana nazo.

Mwakifumbwa anasema licha ya kuishi muda mrefu bila mke, alikutana na Upendo katika mizunguko yake na kujikuta wakianzisha uhusiano kabla ya kuunda familia.

Wawili hao walikutana katika mojawapo ya vikao vya chama cha wasioona, ambako walielewana na kuamua kuishi pamoja mwaka 2020 kabla ya kufunga ndoa rasmi mwaka uliofuata.

“Ni mipango ya Mungu kufanya tukutane na kuwa pamoja katika maisha. Nashukuru tunaishi vizuri, japokuwa wakati mwingine hutokea kutofautiana kwa kauli, lakini siyo kwa ugomvi,” anasema Mwakifumbwa.

“Tunajiheshimu, kuvumiliana na kuaminiana kwa sababu japo sisi ni wasioona, ni binadamu na si wanyama. Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kujiheshimu.”

Mwakifumbwa anasema wanaamini maisha yanawezekana licha ya changamoto wanazopitia, hasa kwa kukosa shughuli rasmi za kipato.

Kama wanandoa wengine, anasema wanakabiliana na changamoto za maisha huku wakimtegemea Mungu kwa matumaini ya kubadilisha hali yao ya baadaye na kuishi kwa faraja.

“Nafurahia ndoa yangu kwa sababu tunashirikiana na kusaidiana mawazo, na maisha yanaendelea. Tumekabidhi maisha yetu kwa Mungu na tunasali kanisani tukiamini kesho yetu itakuwa yenye mafanikio,” anaeleza Mwakifumbwa.

Upendo, kwa upande wake anasema baada ya kuolewa, anajihisi wa thamani katika jamii na familia yao.

Anasema kinachomfurahisha zaidi ni heshima na upendo anaopokea kutoka kwa wana ukoo wake.

“Siwezi kumsaliti wala yeye hanisaliti. Tunaaminiana na hata mmoja wetu akisafiri, tunakuwa na watu wa kutulinda na kutusaidia,” anasema Upendo.

Hawa ni wapenzi wasioona ambao licha ya changamoto ya ulemavu wa macho, wameanzisha mradi mdogo wa kujikimu kimaisha na kujipatia riziki ya kila siku.

Wanandoa hao, kila mmoja akijishughulisha na usukaji wa vikapu, viti na bidhaa za urembo, wanakutana na changamoto ya ukosefu wa soko la uhakika, lakini wanakiri kuwa maisha yanaendelea huku wakiwa na matumaini ya kufanikiwa.

Upendo anasema hajawahi kwenda shule, bali alijifunza kushona kwa kutumia hisia na kugusa mtindo wa ushonaji kupitia marafiki waliomfundisha.

“Sijasoma shule yoyote, lakini hii ni kama kipaji. Nilikuwa najifunza kwa wenzangu kwa kutumia hisia; nilianza kugusa mtindo walivyokuwa wanashona, ndipo nikaanza kujifunza,” anasema Upendo.

“Nilianza kushona soksi, nikaja kwenye mabegi, halafu nikaanza kutengeneza vikapu, shanga za urembo na mikoba kupitia marafiki zangu,” anaongeza.

Wanandoa Upendo Tebela (kushoto) akiwa na mume wake, Andindilile Mwakifumbwa nyumbani pamoja na mtoto wao Agape katika mtaa wa Mbalizi 2 wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya.

Kuhusu upofu wake, Upendo anaeleza kuwa tatizo hilo lilianza tangu akiwa mdogo. Alipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, lakini hakupata nafuu.

“Macho yalianza kuuma, nikapelekwa hospitali na kupewa dawa, lakini hali ikaendelea hadi sasa sioni dalili za kupona,” anasema Upendo.

Kwa upande wake, Mwakifumbwa anasema alianza kuumwa macho akiwa na umri wa miaka saba, na aliweza kuhudhuria shule ya wasioona Katumba, iliyoko Tukuyu, Wilaya ya Mbeya Vijijini.

Anasema licha ya matumaini yake ya kufika mbali kielimu, hakufaulu mtihani wa darasa la saba, hivyo akashindwa kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na mazingira aliyokuwa akiishi.

“Niliishia darasa la saba. Hadi sasa mama yangu ndiye yuko hai, baba alishafariki. Nimekuwa nikijishughulisha na usukaji wa sturi, viti na mikoba kama mke wangu anavyofanya,” anasema Mwakifumbwa.

Mwakifumbwa anasema hawana ulinzi rasmi, lakini wanaishi kwa amani na jamii inayowazunguka, hivyo wanapohitaji msaada wa haraka, hupata usaidizi kutoka kwa jirani yeyote aliye karibu yao.

Kuhusu tahadhari, anasema wamechukua vijana wawili, mmoja wa kike na mwingine wa kiume kutoka kwa ndugu zao ambao huwasaidia kwa karibu katika shughuli zao za kila siku na usimamizi.

“Hatujawahi kutarajia kupata madhara, lakini kwa tahadhari, tuna vijana hawa wawili wanaotusaidia na tunashirikiana vyema na majirani zetu,” anasema.

Mwakifumbwa na mkewe Upendo wanakiri kuwa, ingawa wanakwepa aibu ya kuomba msaada barabarani, wanatamani Serikali iwasaidie sambamba na wadau wengine.

“Upendo anajishughulisha na ushonaji wa mikoba na vitambaa, lakini ana changamoto ya soko na mtaji, hali inayotufanya tuishi kwa tabu,” anasema.

Hata hivyo, anasema mwaka jana Upendo alijiandikisha katika Halmashauri ya Mbeya Vijijini ili kupata mkopo.

Alikamilisha taratibu zote, lakini baadaye dirisha la mikopo lilifungwa. “Nimepanga kurudi kwa kuwa nasikia mikopo imeanza tena ili kuona kama nitapata msaada,” anasema Upendo.

Kwa upande wake, mumewe anaomba msaada wa kupata nyumba kwa vile wanapanga na sasa wanafamilia ya mtoto mmoja.

“Tuna mtoto na tunatarajia kupata watoto zaidi. Kuendelea kuishi kwenye chumba na sebule ni changamoto kubwa. Tunaomba msaada kwa Rais Samia (Suluhu Hassan) na wadau wengine watusaidie kupata nyumba,” anasema Mwakifumbwa.

Pia, anasema mara nyingine wanakosa fedha ya kulipa kodi, lakini mwenye nyumba huwa anawavumilia wakipata wanamlipa.

Jirani wa wanandoa hao,  James Mwasote anasema familia hiyo inahitaji msaada ingawa hawajawahi kuomba hadharani.

 “Hii ni familia ya kupigiwa mfano kwa sababu pamoja na ulemavu wao, bado wameonyesha bidii ya kuyasaka maisha bora,” anasema jirani yao huyo.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Mbeya, Agness Fadhil, anasema anaifahamu familia hiyo na amekuwa akiwasaidia kwa kadri ya uwezo wake.

Anasema alimsaidia Upendo alipoomba mkopo mwaka jana, ingawa baadaye dirisha la mikopo lilifungwa.

Related Posts