Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) inashiriki Maonesho ya “World Travel Market London 2024” ambayo yanafanyika katika jiji la London, Uingereza kuanzia tarehe 5- 7 Novemba, 2024.
Maonesho hayo ambayo taasisi mbalimbali za Wizara ya Maliasili na Utalii zinashiriki, NCAA inatumia fursa hiyo kunadi vivutio vya utalii ikijumuisha uzuri wa asili wa Ngorongoro, wanyamapori wa aina mbalimbali wakiwepo ‘Big 5’, vivutio vya urithi wa utamaduni na mambokale vilivyopo eneo la Ngorongoro ambalo ni Urithi wa Dunia linalotambuliwa na UNESCO.
Mwaka 2023 eneo la Hifadhi ya Ngorongoro lilitangazwa kuwa kivutio bora cha utalii barani afrika ambapo eneo hilo ni moja ya maajabu 7 barani afrika na eneo la kipekee lenye hadhi tatu (03) za kimataifa zinatotambuliwa na UNESCO ambazo ni Urithi wa Dunia mchanganyiko (asili na utamaduni), _Biosphere Reserve na_ _UNESCO Global Geopark_ inayohusisha utalii wa miamba.
Aidha kwa mujibu wa mtandao wa tripAdvisor kwa takribani miaka mitatu mfululizo iliyopita eneo la Ngorongoro lilichaguliwa kama eneo bora kwa watalii waliotembelea (best of the best) kwa wageni wa mataifa mbalimbali wanaotembelea kwa nyakati tofauti.
Ujumbe wa NCAA umeongozwa na Kamishna wa Uhifadhi Dkt. Elirehema Doriye ambapo katika maonesho hayo wanakutana na mawakala wa utalii na wadau mbalimbali kwa ajili ya kunadi vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji zilizopo hifadhi ya Ngorongoro, Soko la Uingereza na mataifa ya ulaya ni moja ya maeneo ya kimkakati wenye wageni wengi wanaotembelea nchi yetu.