NMB yaleta Nondo za Pesa kwa watanzania

KATIKA kuongeza uelewa wa masuala ya fedha kwa maendeleo na ukuaji kiuchumi kwa Mtanzania mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, Benki ya NMB imezindua Programu Endelevu ya Elimu ya Fedha iitwayo NMB Nondo za Pesa, itakayotolewa kupitia vyombo habari, mitandao ya kijamii na makongamano.

NMB Nondo za Pesa imezinduliwa na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi jijini Dar es Salaam Jumatatu ya Novemba 4, ambapo alisema walisema walengwa wa programu hiyo Watanzania wote, lakini kwa upekee, itakuwa na vipengele maalumu vinavyowagusa Vijana na Wanawake.

Mponzi, ambaye alimwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alisema kupitia Nondo za Pesa, benki yake itakuwa inatoa elimu kwenye mada muhimu zote kuhusiana na fedha, ikiwamo namna ya kupanga bajeti, kuweka akiba, uwekezaji, mikopo, bima na mipango mingine ya kifedha.

“Lengo la kusambaza Elimu ya Fedha kwa umma wa Watanzania ni umuhimu wake mkubwa kwa jamii, kukosa elimu hiyo kumewaingiza wengi kwenye changamoto za kimaisha, kiuchumi, kielimu, kiafya. Mikopo kandamizi ‘kausha damu,’ ni zao la ukosefu wa elimu ya fedha, ambayo sisi Taasisi za Fedha ni wajibu wetu.

“Walengwa ni Watanzania wote, ila kwa kipekee tutayagusa makundi ya vijana ambalo linajumuisha asilimia 66 ya Watanzania na wanawake. Kwanini Vijana, ni kwa sababu ni kundi lenye fursa kubwa ya kiuchumi, ingawa tayari tuna jukwaa lao maalum la GOnaNMB, lakini bado tunalenga kuwapa vijana mbinu bora za kifedha.

“Wanawake watafikiwa zaidi na NMB Nondo za Pesa, kwa sababu hawa ni nguvu kuu katika uchumi wa familia na jamii. Pia, wao tunalo jukwaa lao maalum la JASIRI ambalo linawawezesha kwa kuwapa maarifa ya kifedha, akiba, na mikopo salama inayosaidia kuanzisha au kuendeleza biashara zao,” alifafanua Mponzi.

Uzinduzi huo uliohudhuriwa na makundi mbalimbali ya vijana na wanawake, Wanafunzi wa Elimu ya Juu, wajasiliamali, bodaboda, mama na baba lishe, ulienda sambamba na uzinduzi wa kipindi cha runinga kiitwacho The Junction, kitachoruka mara moja kwa mwezi na kutoa elimu ya fedha kwa Watanzania wote.

“Kulingana na takwimu ya Finscope ya Mwaka 2023, mtu mmoja kati ya 10 wenye akaunti za kibenki ndio wanaokopa benki, hii ikatusukuma NMB kuona umuhimu wa Watanzania hususani Vijana na Wanawake, wakajua huduma zetu mahususi ambazo wanaweza kunufaika nazo kwa kuingia tu kwenye mfumo ramsi.

“Nondo za Pesa ni muendelezo wa huduma rafiki za NMB kwa Watanzania, zikiwemo NMB Kikundi Akaunti (ambayo ni maalum kwa vikundi vya kijamii), NMB Jiwekee inayomuwezesha mteja wetu aliye nje ya mifumo rasmi ya ajira kujiwekea akiba, pia tunayo Mshiko Fasta, mkopo usiohitaji dhamana wala ujazazi fomu,” aliongeza Mponzi.

Alitaja huduma zinginea rafiki kwa Watanzania kuwa ni NMB Pesa akaunti isiyo na makato ya mwezi inayofunguliwa kwa Sh. 1,000, Spend to Save inayokupa uhuru wa kujiwekea akiba kulingana na matumizi yako yanayopitia kwenye akaunti yako asilimia utakazojichagulia.

“NMB ni kinara wa mapinduzi ya huduma na Nondo za Pesa itaenda kumnufaisha kila mmoja popote alipo kupitia kipindi cha televisheni, radio, mitandao ya kijamii, makongamano, meseji za dondoo za fedha kwa wateja wetu, madarasa ya elimu za kifedha, kliniki za elimu za fedha kwenye matawi yetu,” alisema Mponzi.

Wakizungumza baada ya uzinduzi huo, Frank Silvester Mrope ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki na Bajaji (CMPD Wilaya ya Kigamboni), alisema amefurahia ujio wa NMB Nondo za Pesa ili kuwajengea uelewa na uwezo wasafirishaji wa chama chake ambao ni wanufaika vinara benki hiyo.

“NMB wamekuwa wadau wetu wakubwa, wametukopesha pesa, lakini pia vyombo vya usafiri kama pikipiki na bajaj, kwa hiyo sisi ni wanufaika wakubwa wa huduma zao na walichofanya hapa ni kutuongezea elimu zaidi za utafutaji na uwekaji akiba kwa faida yetu na vizazi vyetu.

“Wito wangu kwa bodaboda na bajaj ambao wako nje ya vyama, wajitokeze kujisajili ili kuingia kwenye mifumo rasmi ya kibenki, waweze kukopesheka, kwa sababu ni ngumu kwao kupata fursa wakiwa nje ya mifumo” alisema Mrope.

Naye Mussa Julius, ambaye ni Afisa Habari wa CMPD Wilaya ya Kinondoni, aliwapongeza NMB kwa kuwajali na kuwathamini waendeshaji wa bodaboda na bajaj Dar es Salaam kwa kuja na program hiyo, huku akiitaka kuwafuata madereva vijiweni na mitaani kuwapa elimu hiyo, kwani wengi wao hawana elimu ya fedha.

“Tumeipokea NMB Nondo za Pesa, tunaiomba NMB iandae mpango mkakati wa kuwafikia madereva wetu, ambao hawana elimu ya fedha. Tumefikia hatua ya kutokuwa na akiba kubwa, licha ya kuhudumu kwa muda mrefu katika sekta ya usafirishaji, kwahiyo hii ‘project’ tunaamini itakuwa mwarobaini,” alibainisha

Kwa upande wake, Ruth Lema wa Soko la Wajasiliamali la Mbezi kwa Beda, jirani na Stendi Kuu ya Mabasi ya Magufuli, alisema uzinduzi wa NMB Nondo za Pesa umekuja na manufaa makubwa kwao kwani wamejifunza vitu vingi ikiwemo fursa za ukopaji, uwekezaji, bima na masuala mazima ya elimu ya fedha.

“Tumefurahia uzinduzi huu, umetuongezea vitu vingi ikiwemo namna mbalimbali za kukopa, matumizi sahihi na umuhimu wa urejeshaji wa mikopo na fursa zingine nyingi kwa vijana na wanawake. Wito wangu kwa wajasi;iamali wote kujiunga na vikundi vya kijamii na kunufaika pamoja na huduma za NMB,” alisema Bi. Ruth.

Related Posts