Shirika lisilokuwa la kiserikali la Organization for Community Development (OCODE) limetoa mafunzo kabambe ya stadi za maisha kwa wajumbe wa kamati za shule (UWAWA) umoja wa walimu na wazazi sambamba na viongozi wa dini wa Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mafunzo hayo mratibu wa stadi za maisha Wilaya ya Bagamoyo kutoka shirika la Ocode Tunu Sanga amebainisha kwamba lengo la mafunzo hayo ni jinsi ya kuweza kukabiliana na matatizo wanayoyakabili katika maisha yao.
Mratibu huyo amesema kuwa mafunzo hayo ambayo yamefanyika katika shule ya msingi Nia njema yamewashirikisha jumla ya washiriki 37 ambao wamepata fursa ya kujifunza stadi za maisha.
Tunu alisema kwamba shirika lao limeweza pia kuendesha shughuli ya kuto elimu ya stadi za maisha ambapo imefanikiwa kuwafikia wajumbe 109 kutoka maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Bagamoyo.
Alisema katika mafunzo hayo pia wameamua kuwashirikisha na viongozi mbali mbali wa dini ambao wataweza kutoa elimu kwa wananchi wengine kuhusiana na umuhimu wa stadi za maisha.
“Tumekutana na wajumbe wa kamati za shule (UWAWA) sambamba na umoja wa wa walimu na wazazi pamoja na viongozi wa dini ili kuweza kukaa kwa pamoja na kuwapatia namna bora ya kuweza kukuza hizi stadi za maisha ,”alisema Tunu.
Kadhalika Tunu alifafanua kwamba wameweza kufundisha namna ya kujiamini kuwa na ushirikiano,masuala mbali mbali ya kutatua matatizo,heshima pamoja na mambo ya ubunifu.
Naye mgeni rasmi katika mafunzo hayo Afisa elimu maalumu Sekondari Wilaya ya Bagamoyo Frank Kwayu amelipomgeza shirika la. Ocode kwa kuweza kutoa stadi za maisha ambazo zitakwenda kuwasaidia walimu,wazazi na wanafunzi katika kutatua changamoto zao.
Afisa Elimu huyo alisema kwamba shirika la Ocode limeweza kufanya kitu kizuri kwa kuamua kushirikiana bega kwa bega na serikali ya Wilaya ya Bagamoyo katika suala zima la stadi za maisha na kwamba mafunzo hayo yataweza kuwa chachu ya maendeleo.
“Tunashukuru sana kwa wenzetu wa shirika la Ocode kwa kuweza kuja Wilayani kwetu na kuweza kutoa mafunzo juu ya stadi za maisha kwa makundi mbali mbali na sisi tutawapa ushirikiano katika shughuli zao,”alisema Afisa elimu huyo.
Shirika la Ocode kwa sasa limeshafanikiwa kutoa mafunzo hayo kwa zaidi ya wajumbe wapatao 109 na kuweza kuzifikia shule nne nne za msingi katika kutoa elimu hiyo ikiwemo shule ya Msingi Mataya,Bigilo,Ukuni pamoja na shule ya msingi Nia njema zote za Wilaya ya Bagamoyo.