KOCHA wa Singida Black Stars, Patrick Aussems amesisitiza umuhimu wa kutumia mapumziko ya wiki mbili za kalenda ya Fifa kuboresha kikosi ili kukabiliana na ratiba ngumu ya kucheza michezo mitatu ndani ya siku nane.
Singida Black Stars ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikikusanya pointi 23 nyuma ya Yanga yenye pointi 24.
Aussems ambaye baada ya kalenda ya Fifa atakuwa na mechi mbili ugenini dhidi ya Tabora United na Azam, kisha moja nyumbani dhidi ya Simba alisema: “Hii ni nafasi ya kujiandaa vyema kabla ya kipindi kigumu tutakachokabiliana nacho kucheza mfululizo. Tunahitaji nguvu zaidi.”
Kocha huyo raia wa Ubelgiji aliongeza kwamba: “Tumejenga msingi mzuri, lakini tunahitaji kujizatiti kwa sababu tuna ratiba ngumu inayotukaribisha. Kila mchezo ni muhimu na tunapaswa kuingia kwenye mechi hizo tukiwa tayari.
“Michezo hii itakuwa kipimo cha uwezo wetu. Sina shaka kwamba wachezaji wangu wataweza kutoa kiwango cha juu katika kila mchezo, na tunatumai kupata matokeo mazuri.”
Aussems alionyesha imani na wachezaji wake akisema: “Tuna wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu na nina matumaini kwamba watajituma na kuonyesha uwezo kwenye uwanja.”
Kuelekea mechi hizo, kocha huyo aliwataka wachezaji wake kuzingatia mazoezi na kuboresha mchakato wa kiufundi ili kukabiliana na changamoto zinazokuja.
“Tunaweza kushinda michezo hii ikiwa tutakuwa na nidhamu na umoja kwenye uwanja,” aliongeza.
Kwa kuangazia matokeo na kiwango cha mchezo, Singida Black Stars inatarajiwa kuingia kwenye mechi hizo zikiwa na mtazamo wa ushindi, huku Aussems akipambana kuhakikisha kila mchezaji anakuwa katika kiwango bora.
Mchezo kati ya Tabora United dhidi ya Singida Novemba 24, baada ya hapo watakwenda Chamazi kuivaa Azam Novemba 27 kabla ya kuikaribisha Simba Desemba Mosi kwenye Uwanja wa Liti, Singida.
Wakati huohuo, kiungo mshambuliaji wa Singida Black Stars, Marouf Tchakei amesema anaiona timu hiyo ikishiriki michuano ya kimataifa msimu ujao kutokana na ubora wa wachezaji waliopo kikosini.
Tchakei kwenye mechi 10 alizocheza amebakiza bao moja kuvunja rekodi ya msimu uliopita ambao alifunga manne huku msimu huu hadi sasa ameingia kambani mara tatu.
“Tumeanza vizuri msimu tofauti na msimu uliopita, pia kumekuwa na mchanganyiko wa wachezaji wengi bora ambao wana uchu wa mafanikio, naiona timu yangu ikimaliza pazuri na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa,” alisema.
“Kila mchezo kwetu ni fainali na tumekuwa tukichza kwa kujituma lengo ni kupambana kufikia mafanikio ambayo ni kucheza michuano ya kimataifa mwakani kitu ambacho naamini kinawezekana kwa asilimia kubwa kutokana na ubora wa mchezaji mmojammoja na timu kwa ujumla.”
Kuhusu ufungaji bora, Tchakei alisema anapambana kuisaidia timu kufikia malengo, huku ishu ya mabao atakayofunga akiiweka kando kwa madai kwamba ni mapema sana kwake kuzungumzia hilo, lakini atatumia vizuri kila nafasi atakayoipata kufunga.
“Siwezi kusema nitafunga mabao mangapi msimu huu ila nitatumia kila nafasi nitakayoipata, idadi itajulikana mwisho wa msimu na naamini nitakuwa nimevunja rekodi ya msimu uliopita na kuwa mwiongoni mwa wachzaji walioipambania Singida Black Stars kufikia malengo,” alisema.