Na. Asia Singano na Peter Haule, WF, Dodoma.
Serikali imesema kuwa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani imetoa msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye uingizwaji wa vyakula vya mifugo ikiwemo vyakula vya Samaki vinavyotambulika kwa HS Code 23.09 chini ya utaratibu wa utozaji ushuru wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kupunguza kodi ya uingizaji wa vyakula vya samaki nchini.
‘’Vifaa vinavyoagizwa kutoka nje na watu wanaojihusisha na ufugaji wa samaki na kilimo ambavyo Kamishna ameridhika kuwa ni kwa matumizi katika sekta ya ufugaji wa samaki vimeondolewa Ushuru wa Forodha kwa mujibu wa Kifungu cha 15(a) cha Sehemu B ya Jedwali la Tano ya Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, alisema Mhe. Nchemba.
Dkt. Nchemba alifafanua kuwa Serikali inaendela kuongea na sekta ili kuona maeneo ambayo yanastahili kupata ruzuku na tayari baadhi ya maeneo Serikali inatoa ruzuku na itaendelea kutoa ruzuku katika maeneo mbalimbali kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha.
Aliongeza kuwa Serikali inaweka vivutio kwenye uzalishaji wa bidhaa ili kujitosheleza ndani ya nchi ili kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje na kuwa itaangalia maeneo ya maboresho katika bajeti ijayo kufanikisha kuongeza uzalishaji wa ndani.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Jacqueline Ngonyani Msongozi, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kupunguza kodi ya uingizaji wa vyakula vya samaki nchini.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha)