Wapiganaji wa RSF wamevamia miji kadhaa katika jimbo la Gezira, kusini mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum na kuwaua kikatili takriban raia 120 katika mashambulizi ya mfululizo katika maeneo hayo.
Hayo ni kulingana na ripoti tofauti za vyombo vya habari na Umoja wa Mataifa huku vyanzo vingine, vikisema mamia ya watu wamejeruhiwa kutokana na mashambulizi katika siku chache zilizopita.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Misaada ya Kiutu (OCHA) imesema idadi ya watu waliojeruhiwa ni kubwa na zaidi ya 47,000 wameyakimbia makazi yao katika mashambulizi haya ya hivi karibuni.
Mauaji hayo ya karibuni zaidi ni mwendelezo wa ukatili wa vita vilivyozuka Aprili 2023 wakati mvutano kati ya jeshi la Sudan na RSF ulipoanzana kuwa mapigano.
Tangu wakati huo, karibu watu 25,000 wameuawa, kulingana na shirika la takwimu za maeneo na matukio ya kivita ambalo limekuwa likifuatilia mzozo huo tangu ulipoanza.
Soma pia:Pande hasimu Sudan zatakiwa kuruhusu misaada kuwafikia raia
Ripoti iliyotolewa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaofuatilia unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa RSF imehitimisha kwamba kuna ushahidi wa kuridhisha na kuaminika kuwa vitendo hivyo ni uhalifu wa kivita.
Waangalizi wa vita vya Sudan wanasema mashambulizi hayo ya RSF yanachagizwa na kitendo cha aliyekuwa kamanda wao katika eneo la Gezira, Abu Aqla Keikel aliyewaasi na kujiunga na jeshi la Sudan.
Mashirika yathibitisha uhalifu wa kivita
Kulingana na ripoti ya shirika lisilo la kiserikali la Fikra for Studies and Development la Sudan RSF ilotoa maneno yanayosomeka “Muueni kijana Keikel kabla hajawa mkubwa,” maneno ambayo wapiganaji wa RSF walisikika wakiimba miongoni mwa kauli mbiu nyingine zinazotaka kukomeshwa kwa kile walichokiita “wasaliti”.
Shirika la Fikra linasema wanajeshi hao waliua watu 300 katika mji wa Tamboul kwa siku moja ya Oktoba 22 baada ya kufanya shambulio kama hilo katika mji mwingine wa Rufaa siku moja kabla, “na kusababisha vifo vya watu 100, kuwabaka wanawakena kuwateka nyara wasichana na kuondoka nao.
Soma pia:HRW: Wakimbizi wa Sudan wako hatarini nchini Ethiopia
Marina Peter, Mwenyekiti wa Jukwaa la Ujerumani nchini Sudan na Sudan Kusini lakini likiwa na makao yake makuu hapa Ujerumani ameiambia DW kuwa mashambulizi kama hayo kwa bahati mbaya si mageni tena.
Ukatili kama huo ulitokea katika vita vya kwanza vya Darfur mapema miaka ya 2000, alisema.
“Wakati huo pia, kulikuwa na ukatili wa kutisha, watu walichomwa moto hadi kufa, waliotoroka walipigwa risasi, raia waliteswa, na wanawake walibakwa kwa wingi,” aliongeza Marina Peter.
SAF yashutumiwa kwa mauaji
Lakini kwa upande mwingine, Jeshi la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdel Fatah Al-Burhan linatajwa pia kusababisha mauaji mengi kwa raia wa Sudan kwa kuwahamasisha watu wenye silaha kujilinda na kupambana na wapiganaji wa RSF ambao wakosoaji wanasema watu hao hawana uzoefu wa kutumia silaha na hivyo wanaishia kupoteza maisha.
Soma pia:Mashambulizi ya siku mbili ya RSF huko El-Fasher yaua watu 48
Kutokana na hayo, mzozo nchini humo unaendelea kupanuka na inatabiriwa kuwa inaweza kupelekea ghasia katika mataifa jirani kwa kuhusisha makundi yenye silaha yanayoweza kuvuka mpaka na kuzidisha msukosuko katika ukanda huo.
Kwa wakati huu, wataalam wa masuala ya migogoro wanasalia kuwa na mashaka kuhusu upatanishi wa kimataifa nchini Sudan ikizingatiwa kwamba pande zinazozozana zinapata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wahusika wa kikanda ikiwa ni pamoja na mataifa ya Kiarabu na Urusi.