Unguja. Utafiti uliofanywa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) umebainisha sekta ya umma hakuna chombo cha majadiliano kitakachosaidia kuleta uhusiano mwema kati ya wafanyakazi na mwajiri serikalini.
Hayo yamebainika leo Jumanne, Novemba 5, 2024 wakati wa kuthibitisha ripoti ya uhusiano kazini katika sekta za umma Unguja na kuwashirikisha wadau mbalimbali.
Mtaalamu elekezi aliyehusika katika utafiti huo, Dk Cornel Mtaki amesema kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ) hakuna chombo maaalumu cha kusuluhisha migogoro ya wafanyakazi kama ilivyo sekta binafsi kuwapo kitengo cha usuluhishi na uamuzi wa migogoro (DHU).
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Khamis Suleiman Mwalim amesema utafiti wa uhusiano kazini katika sekta ya umma ni juhudi inayosisitiza kuimarisha sehemu za kazi kwa lengo la kuleta maendeleo nchini.
Amesema utafiti huo utasaidia wafanyakazi na waajiri kuondoa changamoto zinazowakabili na kuboresha mazingira ya kazi.
Ofisa Programu Mwandamizi wa ILO, Kanda ya Dar es Salaam, Edmund Moshi amesema lengo la kuandaliwa kwa warsha hiyo ni kuipitia na kuipitisha ripoti ya uhusiano kazini katika sekta za umma kwa wadau mbalimbali ili kupokea maoni na michango yao katika uboreshaji wa ripoti hiyo.
Amesema matarajio yao kwa Serikali ni kupitisha mkataba wa uhusiano kazini kwa lengo la kuimarisha mazingira bora ya kazi ikiwamo mishahara na haki sawa kwa wafanyakazi wote.
Kamishna wa Kazi, Rashid Khamis Othman amesema ofisi yake kwa kushirikiana na ILO itaendelea kuwaelewesha wadau mbalimbali kuhusu utafiti huo uliojikita kusimamia sheria, kanuni na miongozo ya kazi sekta ya umma.
Pia, amesema wafanyakazi na waajiri wanatakiwa kusimamia na kuboresha majadiliano ya pamoja ili kuweka mazingira bora katika maeneo yao kazi.
Katibu Mkuu wa Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (Zatuc), Khamis Mwinyi Mohammed amesema utafiti huo utasaidia kuboresha uhusiano kazini kwa kuwa kumekuwapo na changamoto za mara kwa mara kati ya waajiri na wafanyakazi.
Mkurugenzi Mtendaji Jumuiya ya Waajiri Zanzibar (Zanema), Salahi Salim Salah amesema,“suala la uhusiano kazini ni muhimu, kama mfanyakazi hana uhusiano mzuri mwema na mwajiri hata kazi haziwezi kufanyika kwa umakini.”
Utafiti huo ulifanywa kwa wafanyakazi wa kawaida wa Serikali, wateule, viongozi, wafanyakazi wa mashirika ya umma na vyama vya wafanyakazi wa umma.