Dodoma. Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amesema uwezo wa kuzalisha umeme uliounganishwa kwenye gridi ya Taifa sasa umefikia megawati 2,607 na mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) unachangia karibia asilimia 50 ya umeme huo.
Akizungumza leo Jumanne, Novemba 5, 2024 wakati wa jukwaa la uziduaji linaloendelea Jijini Dodoma, Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati amesema uzalishaji huo wa umeme umeongezeka kutoka megawati 1,605 zilizokuwepo mwaka 2021, hivyo katika kipindi cha miaka mitatu kumekuwa na ongezeko la asilimia 62.
“Ongezeko la uzalishaji wa umeme linatokana na kukamilika kwa mradi wa Julias Nyerere ambao sasa umefikia asilimia 99.2. Sasa megawati 1,175 zinazalishwa kutoka katika mradi huo,” amesema Dk Biteko.
Amesema kwa upande wa miundombinu ya kusafirisha umeme mpaka sasa kuna kilometa 7,745 huku njia za kusambaza umeme zikiongezeka kufikia urefu wa kilometa 187,817.
Katika mkutano huo, Dk Biteko amesema kutokana na umuhimu wa nishati katika maendeleo ya nchi, Serikali itaendelea kuleta suluhu ya kudumu ya upatikanaji wa umeme kwa kuwa na vyanzo vingi na vya aina tofauti.
Aidha, amesema kutokana na mwelekeo wa dunia wa kutumia nishati safi, Tanzania itatumia rasilimali zake kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo ni matokeo ya matumizi ya nishati chafu.
Miongoni mwa rasilimali hizo ni gesi asilia na Dk Biteko ameeleza mpaka sasa ugunduzi wa gesi nchini Tanzania ni futi za ujazo trilioni 57.54 na kati ya hizo trioni 47.4 zimegunduliwa eneo la kina kirefu cha bahari na trilioni 10.12 nchi kavu.
“Ugunduzi wa gesi ni fursa kubwa kwetu wakati tupo kwenye kampeni hii ya mabadiliko ya nishati kwenda kwenye matumizi ya nishati safi, kwani miongoni mwa changamoto kubwa zinazoisumbua dunia hivi sasa ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Dk Biteko.
Hata hivyo, amesema katika mabadiliko hayo ni muhimu kuangalia uhalisia wa kiuchumi wa watu, kwani kwa kiasi kikubwa matumizi ya nishati safi yana gharama kubwa kuliko nishati utumikayo hivi sasa.
“Nishati safi tunaihitaji sana, lakini tutaendelea kutumia nishati nyinginezo kuleta maendeleo, hususani upatikanaji wa umeme. Tutaendelea na vyanzo vya sasa kwa sababu tunahitaji kubadili hali za watu wetu,” amesema Dk Biteko.
Katika jukwaa hilo, Waziri wa Madini, Antony Mavunde amesema Tanzania imeandaa mkakati maalumu wa kuyavuna madini ambao utaleta tija kwa nchi.
Amesema Tanzania inashika nafasi ya tatu Afrika katika uzalishaji wa madini ya kimkakati ya kinywe, ikitanguliwa na Madagascar na Msumbiji na kuwa upo uhitaji wa kuongeza nguvu kwenye uzalishaji huo ili kuwa mzallishaji mkubwa zaidi barani Afrika.
“Tanzania inashika nafasi ya tatu ikizalisha asilimia 0.64 ya mahitaji yote duniani kitanguliwa na Madagascar na Msumbiji, ” amesema Mavunde na kuongeza kuwa rekodi hiyo imewekwa na mzalishaji mdogo, God Mwanga aliyepo eneo la Kwa msisi wilayani Handeni Mkoa wa Tanga.
“Kuna leseni 12 hazijaanza kufanya kazi zikianza kufanya kazi hizi Tanzania itakuwa kinara wa uzalishaji madini ya graphite ya barani Afrika, ” amefafanua Mavunde.
Wakati wa ufunguzi wa jukwaa hilo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Hakirasilimali, Adam Antony amesema wananchi wanapaswa kufurahia uwepo wa rasilimali katika maeneo yao.
Antony amesema taasisi yake ina imani katika uwazi ambao ni chachu ya maendeleo ya sekta ya uziduaji.
“Sekta ya uziduaji ni ya muhimu kwa Taifa na ninapongeza hatua za kisera zinazofanywa na Serikali. Ni muhimu, kwani wananchi wanapaswa kufurahia rasilimali hizo,” amesema.