Dar es Salaam. Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuboresha uwezo wake wa kukopesheka.
Hii ni kutokana na viwango vipya vya ukadiriaji wa mikopo vilivyotolewa na Moody’s Investors Service na Fitch Ratings, kuonyesha mafanikio ya kiuchumi katika Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, viwango hivyo vinaonyesha usimamizi mzuri wa fedha wa nchi pamoja na ukuaji thabiti wa uchumi.
Moody’s imeipa Tanzania alama ya B1, huku Fitch ikiipa alama ya B+, viwango ambavyo vinaifanya Tanzania kuwa juu ya nchi nyingine za Afrika Mashariki za Kenya, Uganda na Rwanda. Akihutubia Bunge Novemba Mosi, 2024, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alisema hadi kufikia Juni mwaka huu, deni la serikali lilifikia Sh96.88 trilioni na deni la nje lilikuwa Sh64.93 trilioni na la ndani Sh31.95 trilioni.
Hata hivyo, tathmini ya uhimilivu inaonyesha deni hilo bado liko ndani ya viwango vinavyokubalika kimataifa.
“Matokeo mazuri ya ukadiriaji wa mikopo kwa Tanzania kutoka Moody’s na Fitch Ratings ni uthibitisho wa juhudi za serikali yetu kukuza uchumi na kuimarisha mazingira ya kifedha yenye ustahimilivu,” amesema Dk Nchemba.
Ukadiriaji wa Moody’s kwa Tanzania unalingana na ule wa nchi nyingine za Afrika zinazoonyesha ukuaji wa kiuchumi kama Namibia, Benin na Senegal, ambazo nazo zimepewa alama ya B1. Ukadiriaji huu unaiweka Tanzania katika orodha ya nchi tano bora kiuchumi Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwa nyuma ya Botswana (A3), Mauritius (Baa3), Côte d’Ivoire (Ba2), na Afrika Kusini (Ba2).
Hii inaonyesha nafasi ya Tanzania kama uchumi unaoongoza Afrika Mashariki, ikiizidi Kenya (B3), Uganda (B2) na Rwanda (B2).
Katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Tanzania iko sawa na Namibia katika kundi la B1, ikizishinda nchi jirani za kikanda.
Kutokana na hilo, Waziri Nchemba alisema mageuzi ya kimuundo katika sekta muhimu, ndiyo yanaimarisha mazingira ya biashara nchini sambamba na kuboresha sekta ya uwekezaji. “Tumetekeleza mageuzi yanayorahisisha biashara, kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika sekta muhimu,” amesema.
Amesema Wizara ya Fedha pia imeweka mkazo katika kuboresha usimamizi wa fedha za umma, ukusanyaji wa kodi na uwazi, mambo ambayo yameakisiwa na tathmini nzuri iliyotolewa na Moody’s.
Wakati huo huo, imeelezwa kuwa ahadi iliyotolewa ya kuendeleza miradi mikubwa ya miundombinu kama wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere na Reli ya Kisasa (SGR), zimeboresha mazingira ya kusaidia shughuli za kiuchumi.
Akizungumza na gazeti dada la The Citizen, mchambuzi mwandamizi wa masuala ya fedha, Dk Thobias Swai amesema viwango hivyo vya mikopo vinaonyesha usimamizi mzuri wa kifedha wa serikali.
Amesema nchi imeweza kukopa kwa masharti mazuri na kwamba ikiwa sera za sasa zitaendelea, matarajio ya muda mrefu yatabaki kuwa chanya.
“Hata hivyo, ni muhimu kuendeleza juhudi za kuongeza ukusanyaji wa mapato ya kodi, mauzo ya nje na uwekezaji katika sekta muhimu zinazochochea ukuaji wa uchumi,” amesema Dk Swai.
Na amesisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu na kuiunganisha vyema na sekta zenye uzalishaji.
“Usimamizi thabiti wa fedha na matumizi ya umma ni muhimu kwa kudumisha mwelekeo huu mzuri,” amesema na kuongeza kuwa ukadiriaji mzuri pia wa mikopo huongeza sifa ya nchi na kuvutia biashara na uwekezaji zaidi.
Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Wilhelm Ngasamiaku amesema viwango hivyo vinaashiria uchumi wa Tanzania unafanya vizuri katika viashiria vikuu vya kiuchumi kama vile ukuaji wa Pato la Taifa (GDP), mfumuko wa bei, uwiano wa akaunti ya sasa na uhimilivu wa deni la taifa.
“Hii ina uwezo wa kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDIs) na kuongeza mtaji wa kigeni nchini, kwani uchumi wenye nguvu una sifa ya kulipa mikopo kwa masharti nafuu,” amesema.
Dk Ngasamiaku pia alimebainisha kuwa viwango bora vya mikopo vinaweza kuongeza akiba ya fedha za kigeni na kuimarisha thamani ya fedha za ndani.
Amesema viwango hivyo pia husaidia kuvutia mashirika ya kimataifa kuanzisha shughuli zao katika nchi zenye uchumi imara na mazingira bora ya biashara.
Mchumi wa Biashara ya Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Lutengano Mwinuka kwa upande wake amesema, taasisi zinazotoa ukadiriaji wa mikopo hutoa tathmini zenye mtazamo wa mbele, jambo ambalo lina manufaa kwa nchi na vyanzo vya mitaji. “Ukadiriaji ambao Tanzania imepata unaakisi uthabiti wa sekta mbalimbali na utendaji mzuri wa uchumi kwa ujumla. Hii ni muhimu kwani kwa muda mrefu nchi imekuwa na ukuaji thabiti wa uchumi unaoendeshwa na sekta muhimu,” amesema Dk Mwinuka.