Dodoma. Mjadala wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, umewafanya wabunge kuibua hoja kadhaa zinazolenga kuimarisha miundombinu ya intaneti, usimamizi wa kodi, na viwango vya huduma za ulinzi.
Wabunge hao waliibua hoja hizo jana jioni Jumatatu, Novemba 4, 2024 wakati wakijadili mapendekezo hayo.
Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga amesisitiza mpango huo utafanikiwa iwapo Serikali itajenga mazingira ya upatikanaji wa uhakika wa intaneti na nishati ya kutosha kwa maendeleo ya sekta za kiuchumi na kijamii nchini.
Sanga amesema hayo wakati wakijadili mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.
Amesema asilimia 90 ya shughuli zinazotegemewa katika mpango huo zinahusiana na uchumi wa kidijitali ambao unaendeshwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Sanga amesema uhakika wa intaneti unategemewa sana na Serikali, sekta binafsi na vijana waliojiajiri kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
“Mipango mingi ya Serikali na sekta binafsi inategemea teknolojia, na Serikali inapaswa kuhakikisha upatikanaji wa intaneti ni wa uhakika,” amesema Sanga.
Katika mchango wake, Sanga amesisitiza upatikanaji wa intaneti wenye kasi na uhakika ni jambo muhimu kwa kufanikisha mpango wa maendeleo, na kwamba tatizo la kukosekana kwa mtandao kwenye baadhi ya maeneo linazuia shughuli za kibiashara na huduma za kijamii.
“Unapokutana na changamoto ya mtandao kuwa chini, hata ulipaji wa huduma mbalimbali kama mafuta au manunuzi unakwamishwa,” amesema.
Amesema kulingana na taarifa, Watanzania milioni 36 wapo kwenye mtandao wa intaneti, huku wengine milioni 12 wakitumia mtandao wa 2G.
Sanga pia ameshauri Serikali inapaswa kuwekeza zaidi kwenye uendelezaji wa mkongo wa Taifa, akieleza mkongo huo utasaidia kuimarisha upatikanaji wa intaneti hadi maeneo ya ndani zaidi ya nchi.
Ametolea mfano wa huduma kama upasuaji wa kimatibabu unaohitaji kushirikiana na hospitali za nje ya nchi, pamoja na ukataji wa tiketi za treni ya SGR, zote zikitegemea intaneti.
Kwa upande wa nishati, Sanga amesema upatikanaji wa uhakika wa nishati ni jambo muhimu kwa ajili ya kuongeza uzalishaji viwandani, kama ilivyopangwa katika mpango wa maendeleo.
Amependekeza kuongeza vyanzo vya nishati mbadala kama vile upepo na kusisitiza fidia kwa maeneo yanayohusika na miradi ya nishati ilipwe kwa wakati.
Sanga ametaja mradi wa bwawa la Lumakali katika jimbo lake la Makete kama mfano wa mradi wa nishati mbadala ambao ukikamilika utaongeza upatikanaji wa umeme kwa viwanda na huduma nyingine za kijamii.
Katika mjadala huo, Mbunge wa Nyang’hwale (CCM), Hussein Amar amezungumzia changamoto za ukusanyaji wa kodi, akiwalalamikia baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao wanashirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu kukwepa kodi.
Amar ametoa mfano wa jinsi baadhi ya mabasi yanayotoa huduma za usafiri mikoani yanavyotoa risiti za mkono badala ya kutumia mashine za kielektroniki (EFD) zinazotakiwa na Serikali.
Amar ameiomba Serikali kubadili utaratibu wa ununuzi wa mashine za EFD na kuzifanya ziwe na gharama nafuu, ili kila mfanyabiashara amudu, badala ya kuweka masharti ya gharama zinazohusishwa na thamani ya biashara ya mtu.
Amependekeza Serikali iagize mashine hizo kiwandani, kisha iziuze kwa wafanyabiashara kwa mkopo au bei nafuu, ili kuondoa changamoto ya matumizi ya risiti za mkono ambazo huleta upotevu wa mapato ya Serikali.
Mbunge mwingine aliyechangia, Almas Maige wa Tabora Kaskazini (Uyui), ameibua hoja kuhusu usimamizi wa kampuni za ulinzi na amesisitiza umuhimu wa kutungwa kwa sheria itakayosimamia uanzishwaji na uendeshaji wa sekta hiyo.
Ameeleza kampuni nyingi za ulinzi zilizopo nchini zinakosa viwango vya kimataifa kutokana na changamoto katika utoaji wa leseni na usajili.
Maige ameeleza kuwa kitendo cha Jeshi la Polisi kumiliki kampuni za ulinzi kunaleta mgongano wa kimaslahi, kwani wao ndio wenye jukumu la kutoa vibali kwa kampuni za ulinzi nchini.
“Jeshi la Polisi linashindwa kuweka viwango au madaraja kwa kampuni, jambo linalosababisha ushindani usiokuwa wa haki kwa kampuni za ulinzi nchini,” amesema Maige.