Dar es Salaam. Watanzania wametakiwa kuzingatia matumizi bora ya umeme kwa kuacha kutumia vifaa vingi kwa wakati mmoja kama havina ulazima ikiwamo pasi, redio na jiko ili kuepuka upotevu wa nishati hiyo.
Rai hiyo inakuja wakati kiango cha upotevu wa umeme kwa sasa nchini ni asilimia 14, kutoka 21 mwaka 2018 huku lengo ikiwa ni kufikia asilimia tisa ambayo ni kiwango cha kawaida cha upotevu.
Hayo yamebainishwa hii leo Jumanne Novemba 5, 2024 jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa vyombo vya habari na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga wakati akitoa taarifa ya mkutano wa kikanda kwa nchi za Afrika Mashariki na za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, (Sadc) unaohusu Matumizi Bora ya Nishati (Reec).
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Desemba 4 hadi 5 mwaka huu jijini Arusha na utahudhuriwa na wadau wa sekta ya nishati wapatao 300 kutoka ndani na nje ya nchi unaotarajiwa kufunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.
Mhandisi Luoga amesema Serikali inaendelea na mikakati ya kuimarisha mifumo ya usafirishaji na usambazaji wa umeme ili kupunguza upotevu wa nishati hiyo muhimu.
“Vivyo hivyo na watu wanapaswa kuzingatia matumizi yaliyo bora, mfano unaweza ukatumia taa zenye Watt ndogo ambazo zina mwanga au jokofu lenye viwango linalotumia umeme kidogo,” ameshauri.
“Kupitia Shirika la Viwango (TBS) na mradi tunaoutekeleza Tanzania wa matumizi bora ya nishati, tumeshaanza kuweka viwango na alama kwenye vifaa vya umeme vinavyoonesha matumizi bora ya umeme,” amesema Mhandisi Luoga.
Mtaalamu wa miradi kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Abbas Kitogo, amesema mradi wa matumizi bora ya nishati unaotekelezwa nchini una lengo la kutengeneza mkakati wa matumizi bora ya nishati.
Lengo lingine amesema ni, “kuweka alama katika vifaa vinavyotumia nishati kwa wingi kwa lengo la kupunguza matumizi na kujenga uelewa kwa wazalishaji wa vifaa hivyo na watumiaji wenyewe.
“Kufadhili mafunzo kwa wahandisi kinadada wanaosoma Chuo cha D.I.T masuala ya uhandisi wa nishati na kujenga uwezo wa matumizi ya ubora wa nishati kwa maofisa wa Serikali na sekta binafsi,” amesema.
Massimiliano Pedretti kutoka Umoja wa Ulaya (EU), amesema katika utekelezaji wa mradi huo, watawasaidia vijana wenye bunifu zinazosaidia matumizi bora ya nishati.