Duru za kitabibu na vyombo vya habari kwenye Ukanda wa Gaza zinasema mashambulizi ya anga na ardhini yaliyofanywa na jeshi la Israel yamesababisha mauaji hayo ya makumi ya Wapalestina na uharibifu mkubwa wa mali.
Makombora yaliyofyetuliwa na ndege za kivita za Israel yameharibu nyumba mbili za makaazi kwenye kitongoji cha Beit Lahiya kaskazini mwa Gaza.
Hayo ni kulingana na shirika rasmi la habari la Kipalestina WAFA pamoja na vyombo vya habari vilivyo chini ya kundi la Hamas. Eneo hilo la Beit Lahiya limekuwa likilengwa na mashambulizi ya jeshi la Israel tangu Okotba 5.
Vyombo vya habari vya ukanda huo vinasema tangu jana jioni hadi mapema leo asubuhi, jumla ya Wapalestina 20 wameuawa kwenye eneo hilo. Watu wengine wanne wameuawa kwenye mji wa katikati mwa Gaza wa Al-Zawayda, hayo ikiwa ni kulingana na duru za kitabibu eneo hilo.
Maafisa wa afya wa Palestina wamesema watu wengine 6 pia wameuawa kufuatia mashambulizi mawili ya anga ya Israel kwenye mji wa Gaza na kitongoji jirani cha Deir Al-Balah.
Israel yasema imewalenga “magaidi” na kukanusha madai ya kuugawa Ukanda wa Gaza
Jeshi la Israel lenyewe limesema bila kutoa maelezo mapana, kwamba vikosi vyake vimewaangamiza wale ilowataja kuwa “magaidi” katika mwa Ukanda wa Gaza na eneo la Jabalia.
Taarifa ya jeshi hilo imesema pia askari wake wamegundua shehena ya silaha na vilipuzi hapo jana kwenye mji wa Rafah kusini mwa Gaza.
Wapalestina wanaituhumu Israel kwamba inalenga kutumia mashambulizi inayoyafanya sasa kuwahamisha watu kutoka maeneo mawili makubwa kaskazini mwa Gaza ili kupata eneo la kuweka vikosi vyake katikati ya pande mbili za ukanda huo.
Madai hayo yamekanushwa na Israel inayodai kwamba oparesheni yake inawalenga wapiganaji wa Hamas na kuharibu miundombinu ya kijeshi ya kundi hilo.
Blinken airai Israel kuongeza misaada kwenye Ukanda wa Gaza na kulikosoa kundi la Hamas
Hayo yakijiri, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken ametoa mwito wa kupelekwa msaada zaidi wa kiutu kwenye Ukanda wa Gaza ikitiliwa maanani kwamba hali ya kibinadamu kwenye eneo hilo imezidi kuzorota zaidi ya mwaka mmoja tangu kuzuka kwa vita.
Blinken ametoa rai hiyo alipozungumza kwa njia ya simu na Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant. Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Blinken imesema, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani amehimiza haja ya kuongezwa msaada wa kiutu unaoingizwa ndani ya Gaza ikiwemo chakula, madawa na mahitaji mengine ya kila siku.
Ikumbukwe Israel ndiyo inaratibu kiwango cha mahitaji yanayoingizwa kwenye Ukanda wa Gaza kupitia vivuko vya ardhini na hata misaada inayofikishwa kwa kurushwa ya maparashuti.
Kwenye mazungumzo hayo Blinken pia amekumbusha umuhimu wa vita hivyo kufikia mwisho na kurejeshwa nyumbani kwa mateka wote wa Israel waliochukuliwa Oktoba 7 mwaka jana.
Hapo jana Blinken pia alizungumza na mwenzake wa Misiri Badr Abdel-Atty kuhusiana na mzozo wa Gaza na hali jumla ya usalama kwenye kanda ya Mashariki ya Kati.
Kwenye mazungumzo hayo Blinken amelilaumu kundi la Hamas kwa kuweka kigingi katika jitihada za kumaliza vita akisema kundi hilo limekataa kuwaachia huru hata mateka wachache wa Israel ili kufungua njia ya kupatikana makubaliano ya kusitisha mapigano.