WAZIRI KOMBO AFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA CUBA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amefanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Cuba, Mhe. Bruno Rodriguez Parrilla jijini Havana, Cuba tarehe 4 Novemba, 2024.

Mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo,sekta ya afya, teknolojia, dawa na vifaa tiba, masuala ya uhamiaji, Utalii, uwekezaji, biashara, utamaduni Sanaa na michezo na elimu.

Kwa upande wa Waziri Kombo amemshukuru mwenyeji wake kwa ukarimu na mapokezi mazuri aliyopata pamoja na ujumbe wa Tanzania unaoendelea kuwasili nchini humo ikiwa ni siku chache za maandalizi kuelekea Ziara ya Kitaifa ya siku tatu (3) ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Cuba kuanzia tarehe 6 hadi 8 Novemba, 2024.

Vilevile, ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na Cuba ikiwa ni pamoja na kuunga mkono jitihada zake za kupinga vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Cuba ili kwa pamoja nchi hizo ziweze kutekeleza kwa tija program za ushirikiano wa kimaendeleo.

Naye Mhe. Parrilla ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono Cuba katika mapambano ya kupinga vikwazo vilivyowekwa na Marekani. Pia aliongeza kuwa Cuba imefurahishwa na msimamo wa Tanzania uliotolewa hivi karibuni kupitia hotuba ya Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa ambapo Tanzania iliunga mkono azimio lingine la Umoja wa Mataifa la kupinga vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba

‘’Tunamsubiri Rais Samia awasili nchini Cuba kwakuwa maandalizi yameshakamilika na kupitia ziara hii tuna imani kwamba ushirikiano wetu utazidi kuimarika. Pia fursa zitakazoletwa na kongamano la kimataifa la Kiswahili litaifanya Cuba kuwa kitovu cha lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Caribbean na sasa vyuo vikuu vya Cuba vimeanza kufundisha lugha ya Kiswahili kama moja ya somo la lugha ya kigeni.’’ alieleza Mhe. Parrilla.

Tanzania na Cuba ni washirika wa muda mrefu, tangu enzi la ukombozi wa bara la Afrika ambapo ushirikiano huo umeziwezesha nchi hizo kuendelea kuthamini na kusimama pamoja katika masuala mbalimbali yaliyopelekea kuichagua Cuba kuwa mwenyeji wa kongamano la Kiswahili litakaloenda sambamba na uzinduzi wa kamusi ya kispanyola – kiswahili wakati wa Ziara ya Kitaifa ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Viongozi wengine walioambatana na Mhe. Waziri Kombo ni pamoja na Balozi wa Jamhuri ya Muungano waTanzania nchini Cuba, Mhe. Humphrey Polepole, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi Naomi Mpemba na maafisa waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba.








Related Posts