MSHAMBULIAJI wa Fountain Gate, Abalkassim Suleiman amesema anajutia kitendo cha kuonyeshwa kadi nyekundu katika mchezo wa juzi dhidi ya Pamba, huku akiweka wazi, ndio chanzo kikubwa cha kikosi hicho kupoteza kwa kufungwa kwa mabao 3-1.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Manyara, mshambuliaji huyo alipata kadi nyekundu dakika ya 39, baada ya kumchezea madhambi ya kumkanyaga nyota wa Pamba, Paulin Kasindi na kusababisha Fountain kucheza pungufu.
“Ni tukio ambalo limeniumiza sana kwa sababu kutoka kwangu kulishusha morali ya wachezaji wenzangu kupambana, nitumie nafasi hii kuomba radhi kwao na benchi letu la ufundi kwa yote yaliyotokea kwani haikuwa kusudio langu kufanya hivyo.”
Nyota huyo mwenye mabao mawili ya Ligi Kuu Bara hadi sasa na kikosi hicho aliongeza, mbali na kusababisha timu hiyo kupoteza, ila kadi nyekundu aliyopata imeharibu pia rekodi yake, kwa sababu alikuwa hajawahi kuonyeshwa maishani mwake.
“Tangu nimeanza kucheza soka la ushindani hii ndiyo kadi yangu nyekundu ya kwanza kuonyeshwa, najutia lakini imenionyesha ni jinsi gani nazidi kukua kiakili na kimwili, nashukuru kwa kila jambo linalonitokea maishani mwangu.”
Nyota huyo aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Mtibwa Sugar, anakuwa mchezaji wa saba msimu huu kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya Cheikh Sidibe (Azam FC), Saleh Masoud (Pamba FC), Victor Sochima (Tabora United), Ibrahim Elias kutoka KMC.
Wengine ni kipa wa Maafande wa JKT Tanzania, Denis Richard na beki wa kati tegemeo wa mabingwa watetezi Yanga, Ibrahim Hamad ‘Bacca’.
Kichapo hicho kwa Fountain kinaifanya timu hiyo kupoteza mchezo wa nne msimu huu kati ya 11 iliyocheza, ikishinda mitano na kutoka sare miwili na safu ya ushambuliaji imefunga mabao 20 na kuruhusu 20, ikiwa nafasi ya tano na pointi 17.