Anayedaiwa kumteketeza mkewe kwa moto aibua mpya mahakamani

Dar es Salaam. Mshtakiwa anayekabiliwa na kesi ya mauaji akidaiwa kumuua mkewe kisha kumteketeza kwa moto kwa kutumia gunia zima la mkaa, Hamisi Said Luwongo, amewataka mawakili wake wasiwakatishekatishe mashahidi wa upande wa mashtaka wakati wakitoa ushahidi, bali wawaache kuwa huru.

Licha ya kuwa na jopo la mawakili watatu wanaomwakilisha, pia mshtakiwa huyo ameiomba mahakama impe nafasi ya kuwahoji mashahidi hao maswali ya dodoso.

Hata hivyo, mahakama imemtaka awaandikie mawakili wake maswali hayo kwenye karatasi, ambao ndio watayauliza wakiona yanafaa, huku ikimpa uhuru wa kuwakataa kama hawaamini.

Mshakiwa huyo ameibua hayo jana, Jumanne, Novemba 5, 2024, wakati wa usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga waMahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.

Hamisi, mkazi wa Gezaulole, wilayani Kigamboni, jijini Dar es Salaam anakabiliwa na kesi ya mauaji ya mkewe Naomi Ernest Marijan, kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kana ilivyorejewa mwaka 2019, akidaiwa kutenda kosa hilo Mei 15, 2019.

Hili ni tukio lililovuma kufuatia taarifa zilizoelezwa na Jeshi la Polisi kuwa mshtakiwa baada ya kumuua mkewe, alimchoma kwa moto mpaka akateketea akitumia mkaa gunia zima, kisha akayazika majivu yake shambani na kupanda mgomba mahali alipoyazika.

Julai 24, 2024, mahakama hiyo ilitoa amri mshtakiwa huyo akafanyiwe uchunguzi wa akili, wakati akitenda kosa analotuhumiwa, kufuatia maombi yaliyotolewa na wakili wa mshtakiwa huyo, Mohamed Majaliwa Septemba 6, 2023, wakati wa usikilizwaji wa awali na kuungwa mkono na waendesha mashtaka.

Jumatatu, Novemba 4, mahakama ilipokea ripoti ya uchunguzi wa afya ya mashtakiwa huyo ambayo imebainisha wakati akitenda kosa hilo alikuwa na tatizo la kiakili.

Hata hivyo, licha ya ripoti hiyo kubainisha hivyo  mahakama iliona ni busara kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo ambapo jana ilianza kupokea ushahidi wa mashahidi wawili wa upande wa mashtaka na leo Jumanne imepokea ushahidi wa mashahidi wanne.

Baada ya shahidi wa nne wa upande wa mashtaka, kumaliza kutoa ushahidi wake wa msingi (akiongozwa na mwendesha mashtaka), mshtakiwa alinyoosha kidole juu huku akimuangalia Jaji.

Jaji Mwanga alipomuona kwanza alimkumbusha kuwa ana mawakili wanaomwakilisha, ambao kama ana jambo ndio alipaswa kuwaeleza na wao ndio waiombe mahakama.

Hata hivyo, alimpa nafasi kumsikiliza ndipo mshtakiwa huyo kwanza aliomba radhi kwa hicho alichokifanya kama atakuwa amekosea, ndipo akatoa hoja yake.

“Ila naomba wakili asimkatishe shahidi wakati anazungumza.Wampe shahidi uhuru wa kuzungumza kile ambacho ana kijua, asimfundishe anavyotakiwa kwenda, kwa sababu anatakiwa azungumze kile anachokijua ili ipatikane haki iliyonyooka,” amesema Luwongo.

Baada ya hoja hiyo ndipo pia akaomba apewe nafasi kuwahoji mashahidi wa upande wa mashtaka maswali ya dodoso yeye mwenyewe.

“Mheshimiwa Jaji lakini pia kama itawezekana naomba nipatiwe nafasi ya kuuliza maswali mawili matatu kwa mashahidi kama, inaruhusiwa kisheria na samahani sana kwa hilo,” amesema Luwongo.

Hata hivyo, Jaji Mwanga amemjibu kwa kuwa tayari ana mawakili wanaomwakilisha basi kama atakuwa na swali au maswali, anaruhusiwa kuyaandika kwenye karatasi na kuwapatia mawakili wake na kwamba wakiona yanafaa watauliza, wakiona hayafai hawatayauliza kwa kuwa wao wanaijua sheria vizuri.

Katika kesi hiyo, mshtakiwa huyo anawakilisha na jopo la mawakili watatu, ambao ni Mohamed Majaliwa, Fatuma Abdul na Jaquim Kamuli, huku Jamhuri ikiwakilishwa na jopo la waendesha mashtaka wanne, linaloongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Yasinta Peter.

Hata hivyo, Jaji Mwanga amempa uhuru kwamba kama anaona mawakili wake hawafai, anaweza kuwakataa na akawatafuta wengine kwa kuwa hilo linaruhusiwa.

Lakini Jaji Mwanga alipomuuliza kama bado anawahitaji au la, mshtakiwa huyo amejibu kuwa ataendelea nao haohao.

Baada ya kuridhia mawakili hao kuendelea kumwakilisha, Jaji Mwanga amemwelekeza mshtakiwa huyo kama atakuwa na jambo lolote, asisimame moja kwa moja kabla ya kuomba ruhusa kwanza.

Kwa kuwa tayari shahidi huyo alikuwa ameshamaliza awamu ya kwanza ya ushahidi wake, yaani ushahidi msingi alioutoa akiongozwa na mwendesha mashtaka, Jaji Mwanga amemruhusu wakili wa mshtakiwa, Majaliwa kuendelea kumhoji shahidi huyo maswali ya dodoso kuhusiana na maelezo ya ushahidi wake.

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Jumatano hii Novemba 6, 2024 kwa mashahidi wengine wa Jamhuri

Kwa mujibu wa maelezo ya awali ya kesi aliyosomewa mshtakiwa, pamoja na ushahidi wa upande wa mashtaka kupitia mashahidi wake walioitwa mahakamani katika ndoa yao yeye na marehemu mkewe walibahatika kupata mtoto mmoja aitwaye Grecious.

Mei 19, 2019 Hamisi alitoa taarifa katika kituo cha Polisi Mjimwema na katika maeneo mbalimbali wakiwemo ndugu wa marehemu, kuwa mkewe huyo alikuwa ameondoka kwenda kusikojulikana na kumwacha mtoto kuanzia Mei 15, 2019.

Julai 16, katika Kituo Kikuu cha Polisi, wakati akihojiwa na ofisa wa Polisi mshtakiwa alikiri kumshambulia na kumuua mkewe Mei 15, 2019 ndani ya nyumba yao kisha akauchukua mwili wake na kwenda kuuchoma moto katika banda lililikuwa limeandaliwa, kwa kutumia mkaa na vitu vingine alivyokuwa ameviandaa.

Katika kukiri kwake huko pia alielezea namna alivyoondoa majivu na masalia mengine kwa kutumia gari lake aina ya Subaru Forester lenye namba za usajili T 206 CEJ mpaka shambani kwake katika kijiji cha Marogoro, wilayani Mkulanga, mkoani Pwani.

Huko shambani aliyazika majivu na masalia hayo katika mashimo yaliyokuwa yameandaliwa kisha akapanda migomba.

Siku hiyohiyo, Julai 16, 2019 mshtakiwa aliongozana na maofisa wa polisi na maofisa wengine mpaka eneo la tukio (nyumbani) na kisha shambani ambako ofisa kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, alichukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba (DNA).

Matokeo ya uchunguzi wa sampuli hizo yalionesha majivu yale yalikuwa ni ya binadamu ambayo yalioana na baadhi ya ndugu wa marehemu Naomi.

Kisha maelezo ya ziada ya mshtakiwa yalichukuliwa na mlnzi wa amani (hakimu wa Mahakama ya Mwanzo), kisha baadaye mshtakiwa alipandishwa kizimbani na kusomewa kosa la mauaji.

Related Posts