Moshi. Kama umewahi kusikia eneo la dhambi limegeuka la wokovu, basi huwezi kuacha kulitaja eneo la Ashira.
Eneo hilo lililopo Marangu, wilayani Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro kwa mujibu wa wakongwe wa mkoa huo, ndilo lililotumika kama kichaka cha kutupa maiti za watoto waliozaliwa na ulemavu au pacha, baada ya kuuawa.
Lakini baadaye, lilitumika na wamisionari kwa ajili ya kueneza dini ya Kikristo na hivyo kulibadili kutoka uwanja wa ukatili dhidi ya watoto hadi kuwa jukwaa la uongofu.
Ashira si jina geni kwa sasa katika ukanda wa Marangu, Jimbo la Vunjo na umaarufu wake unatokana na uwepo wa Shule kongwe ya Sekondari ya Wasichana ya Ashira.
Katika miaka ya 1880, eneo hilo lilitumika kutupa miili ya watoto wachanga waliouawa kwa sababu mbalimbali, kama inavyosimuliwa na Mzee Winford Mosha, mkazi wa Marangu.
Anasema si watoto wachanga pekee, eneo hilo zilitupwa pia maiti za watu wengine kabla ya kuanza kwa utaratibu wa kuzika kwa kufukia kaburini.
Kwa sababu ya shughuli hizo, anasema eneo hilo ilitoka harufu kali na mbaya iliyosababisha kila mmoja kupachukia.
“Zamani wakizaliwa watoto pacha mmoja lazima auawe na hii ni kwa sababu ya woga wa mizimu na wakishauawa hutupwa eneo lile la Ashira, hata walipokufa watu wengine walitupwa pale hivyo palikuwa pananuka sana,” anasema.
Anasimulia jina Ashira lilitokana na neno la Kichaga ‘A-shir’aa lenye maana ya harufu mbaya au vitu vinavyonuka.
Hivyo kutokana na kutupwa maiti ambazo zikioza hutoa harufu kali ndiyo pakaitwa Ashira. “Hili jina A-Shir’aa badaye lilibadilika hadi kuwa Ashira, baada ya Wazungu kushindwa kulitamka ilivyostahili.
Baadaye miaka ya 1890, wamisionari wa kwanza walipofika eneo la Mamba Marangu, walienda kwa viongozi wa kimila wa eneo hilo (Machifu) ili wapewe kwa ajili ya kueneza injili.
“Walipokuja wamisionari wa kwanza katika eneo hili la Marangu walienda kwa mangi (Chifu) wa mamba wakitafuta eneo la kukaa wakieneza injili, wale wazee waliwaogopa kwa sababu waliona watu weupe na hawakuelewa kama watakuwa ni marafiki wazuri au wabaya,” anasema.
Anaongeza kuwa, “Hivyo wazee walikutana na walichokifanya walikubaliana wawapeleke eneo hilo ambalo lilikuwa likitupwa maiti ikiwemo za watoto wadogo na lilikuwa na wanyama kama fisi, wakaona wawapeleke pale.”
Anasema eneo hilo kwa sasa limekuwa na harufu njema ambapo palitumika kutangaza injili na baadaye kujengwa shule ya wasichana ambayo ni moja ya shule kongwe za sekondari nchini.
“Pale badala ya kutoa harufu mbaya inayonuka pametoa harufu njema na habari njema za Yesu Kristo, na kutokea hapo ndipo neno la Mungu lilienea maeneo ya Marangu na baadaye pakajengwa shule ya sekondari ya wasichana,” anasema Mosha.
Stiwart Lyatuu anaeleza hata watu waliokufa vitani wakati wa vita zamani walitupwa eneo hilo la Ashira hali iliyosababisha eneo hilo kupuuzwa na kudharaulika.
“Wakati Wazungu wanakuja, Mamangi (Machifu) wakaona wawape eneo hilo kwa sababu lilionekana ni eneo la mizimu na waliwapa ili kueneza injili na kuondoa mizimu ya watu” anasema Lyatuu na kuongeza.
“Na Wamangi (Machifu) walikuwa hawatoi eneo zuri kwa Wazungu, walitafuta maeneo yasiyoheshimika kwenye jamii na ndiyo maana waliwapa eneo hilo la Ashira ambalo lilionekana linanuka na halifai kwa jamii” anasema.
Akisimulia Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki wa Kanisa la Kiinjili ka Kilutheri Tanzania (KKKT), Mchungaji Calvin Koola anasema zama za ukoloni kabla ya dini kuingia, eneo hilo liliogopwa na wananchi wakidhani kuna mizimu.
“Eneo hili lilidharaulika sana kwa kuwa lilionekana linanuka kwa sababu ya miili ya watu waliokufa iliyokuwa ikitupwa na kuzikwa hapo,” anasema.
Anasema wakati huo, watu hawakuzika katika maeneo mengine kutokana na imani kuwa, kufanya hivyo ni kuiruhusu mikosi.
Anaeleza kuwa wakati wamisionari wamepewa eneo hilo, walijenga kanisa na kutenga eneo kwa ajili ya kuzikia na wakati huo watu wote waliokufa katika maeneo hayo, walizikwa hapo.
Anasema hadi leo katika eneo hilo pametengwa eneo la makaburi hivyo watu wa eneo hilo wanakwenda kuzika wapendwa wao hapo.
“Mwaka 1893 ndipo Kanisa la KKKT Ashira lilianza kujengwa na baada ya dini kuingia ile desturi ya watu kutupa maiti ilianza kupotea, kadri siku zilipoenda dini ilienea na ile hofu ya kuogopa makaburi nayo ilipotea na watu wakaanza kuzika nyumbani.
“Sasa kutoka eneo lililonuka hadi eneo la thamani la Ashira ambako palijengwa kanisa kubwa na baadaye shule kubwa ya wasichana ya sekondari ambayo ilichochea kasi ya maendeleo katika ukanda huo na nchini kote,” anasema.
Maria Joseph anasema eneo hilo kwa sasa limebaki kuwa la kihistoria. “Hata ndani ya shule ya wasichana Ashira karibu na mabweni kuna makaburi.
Anasema zamani kulikuwa na tamaduni nyingi za ukandamizaji hali ambayo ilifanya baadhi wanajamii kuogopa watu waliokufa na hata makaburi.
Mwalimu Koletha Kaale ambaye alifundisha katika Shule ya Sekondari Ashira kwa zaidi ya miaka 28, anasema mpaka leo lipo eneo lililotengwa kwa ajili ya makaburi na watu huenda kuzika.
“Simulizi ya pale ni kwamba palikuwa panatupwa na kuzikwa watu ikiwemo vijana ambao hawajaoa au wasichana ambao hawajaolewa, hivyo palikuwa pananuka lakini baadaye walipokuja wamisionari palijengwa kanisa na shule na mpaka leo ukifika pale utakuta makaburi ya zamani na eneo la makaburi ambalo watu wanaendelea kuzikana lipo,” anasema.