Benki ya Equity Tanzania Yasaini Mkataba wa Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi.


Benki ya Equity Tanzania jana tarehe 5 Novemba 2024, imesaini mkataba na Taasisi ya ADC Tanzania, washauri wabobezi wa biashara, kuashiria kuanza kwa utekelezaji wa mradi maalum wa kuwawezesha wanawake kiuchumi. Mradi huu unafanyika kwa ushirikiano na Taasisi ya Maendeleo ya Kimataifa ya African Guarantee Fund/AFAWA.

Lengo kuu la mradi huu ni kuwajengea wanawake uwezo katika biashara zao ili waweze kufikia vigezo vya kupata huduma mbalimbali za kifedha, ikiwemo mikopo inayotolewa na Benki ya Equity, ili kuboresha maisha yao kijamii na kiuchumi. Huu ni sehemu ya mpango mkakati wa Benki ya Equity wa kuongeza wigo wa huduma kwa wateja wadogo na wa kati (MSMEs), kwa lengo la kufikia 65% ya mikopo yote ifikapo mwaka 2030.

“Tukiwa na dhamira ya kuwawezesha wanawake katika biashara, ushirikiano huu ni hatua muhimu ya kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wanawake wajasiriamali na kuwawezesha kufikia ukuaji wa kiuchumi endelevu,” alisema Leah Ayoub, Meneja Mkuu wa Biashara wa Benki ya Equity Tanzania.

Mradi huu unalenga kuwawezesha zaidi wanawake nchini Tanzania kwa kuwapatia mafunzo ya elimu ya fedha, mikopo nafuu, na ushauri maalum wa biashara.

Kwa hatua hii, Benki ya Equity Tanzania inaendelea kujitolea kuimarisha uimara wa kiuchumi na ujumuishi wa kijamii nchini. Matangazo zaidi ya hatua za mradi huu yatafuata kadri mradi unavyosonga mbele.

Related Posts