GRUMETI FUND YAJIVUNIA KUWAFIKIA VIJANA ZAIDI YA ELFU 20 MKOANI MARA

SHIRIKA la Grumeti Fund kupitia Idara ya Maendeleo ya jamii limejivunia mafanikio yake katika kutoa elimu ya kijinsia kwa vijana wa kike na wa kiume zaidi ya elfu 20 katika Wilaya za Serengeti na Bunda Mkoani Mara jambo linalosaidia kujenga jamii yenye ushirikiano wa pamoja kati ya vijana wa kike na kiume na hatimae kujenga jamii yenye usawa miongoni mwa vijana wa jinsia zote.

 

 

Kwa takribani miaka saba Shirika hilo limekuwa likitoa elimu ya kijinsia kwa wanafunzi wa kike na kiume katika shule za sekondari mbalimbali Wilayani Serengeti na Bunda ambapo tangu mwaka 2017 hadi kufikia Mwaka huu 2024  limefanikiwa kutoa elimu ya kijinsia kwa wasichana 15,352 na kutoa taulo 15,352 kwa kila binti anayeshiriki mafunzo hayo, huku ikifanikiwa kutoa mafunzo kwa wavulana zaidi ya 7,473 tangu mwaka 2021 hadi mwaka huu 2024 na kutoa zawadi za jezi na mipira  kwa kila shule iliyoshiriki kwenye kongamano.

 

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kutoka Grumeti Fund Bi. Frida Mollel akizungumza katika hafla ya kuwakaribisha wageni kutoka nchi mbalimbali waliotembelea Shirika la Grumeti Fund kama hatua ya kushuhudia na kuunga mkono jitihada za Shirika hilo katika kuwapa mabinti elimu ya kujitambua maarufu kama (SERENGETI GIRLS RUN) amesema wageni hao wamekuja kuunga mkono jitihada za Grumeti Fund ili kupata nguvu zaidi na kutanua wigo katika kumkomboa mtoto wa kike katika maeneo mbalimbali hususani katika kupata haki ya elimu na mahitaji muhimu wakati wa hedhi.

 

Aidha Bi. Frida ameongeza kuwa Grumeti Fund inajivunia makongamano mbalimbali ambayo yamekuwa yakifanywa na Shirika hilo kwani yameonesha mabadiliko makubwa katika jamii sambamba na kuwapa nguvu watoto wa kike na wa kiume katika kupambania ndoto zao na kubadili mitazamo hasi katika jamii na kutoa wito kwa jamii kuzingatia usawa baina ya mtoto wa kike na wa kiume ili kujenga jamii endelevu na yenye usawa.

 

“Grumeti Fund imekuwa ikiongea na kutoa fursa kwa  vijana kushiriki kutoa mawazo yao ni kwa jinsi gani wanaweza kuzishinda changamoto zinazowakabili. Tumekuwa  tukiwashauri na kuonesha umuhimu wao katika jamii ili waje kuwa kizazi bora kwani tunaamini kwamba jamii yenye usawa ndani yake ni jamii yenye maendeleo, leo mabinti wameonesha jinsi ambavyo wamenufaika na semina zetu, wameonesha nguvu na ujasiri hivyo natoa wito kwa Jamii kumchukulia mtoto wa kike sawa na wa kiume kwamba wote wanastahili kupendwa na kupewa nafasi ya kupata elimu tusiwe na tabia ya kubagua watoto” ,alisema Bi. Frida.

 

Kwa upande wa wanafunzi wa kike walioshiriki hafla hiyo wameeleza mafanikio makubwa waliyopata kupitia semina mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa na Grumeti Fund na kueleza namna ambavyo zimebadisha fikra zao na kuamsha ari na ujasiri katika kupambania ndoto zao na kuhamasisha usawa katika jamii.

 

 

Related Posts